BANDA AIPA SIMBA MASHARTI MAGUMU

KIUNGO wa Simba, Abdi Banda, amewapa viongozi wa klabu hiyo masharti magumu ili aweze kuongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia timu yao.

Banda alisajiliwa na Simba katika misimu miwili iliyopita ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, akitokea Coastal Union, iliyoshuka daraja msimu uliopita.

Akizungumza na BINGWA jana, mmoja wa viongozi wa Simba, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema baada ya kukutana na mchezaji huyo kujadili mkataba mpya aliweka wazi juu ya masharti aliyoyaweka.

Alisema masharti aliyowawekea viongozi wa Simba ni kwamba, wahakikishe katika mechi tatu wanazocheza ni lazima apate angalau  nafasi moja ya kucheza.

Mtoa habari wetu alisema Simba wakikubali hilo atakuwa tayari kusaini, kwani malengo yake ni kutaka kutunza kiwango chake cha soka.

“Ni kweli kabla ya kuondoka kwao mchezaji huyo alikutana na viongozi kuzungumzia suala la kumuongezea mkataba na ameweka wazi masharti anayoyahitaji ili asaini mkataba,” alisema.

BINGWA lilipomtafuta Banda ili kujua msimamo wake, alisema kwa sasa yupo mkoani Tanga akiendelea na mapumziko na kuhusu mkataba wake Simba, umebaki miezi sita.

“Kwa sasa nawasikilizia Simba, ambao wameonyesha nia ya kuniongezea mkataba, hizo taarifa nyingine kwamba Yanga wananitaka nazisikia tu, hiki ni kipindi cha usajili, yanazungumzwa mengi, lakini mwisho wa siku kila kitu kitajulikana,” alisema Banda.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*