BALE? NI RONALDO NA MADRID YAKE

Madrid, HISPANIA


 

Inawezekana hata wewe msomaji wa kolamu hii ya Super Sub, ulishangaa kusikia kauli ya Ronaldo baada ya Real Madrid kufanikiwa kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya tatu mfululizo.

Kauli ile ilibeba taswira mbili kwa Ronaldo, huku kila moja ikiwa na sababu zake za msingi kabisa katika maisha yake ya soka na mengine.

Kwanza, Ronaldo hakuwa stori kubwa siku ya ubingwa huo kama ilivyozoelekea, hakuwa na njia nyingine ya yeye kuzungumzwa zaidi ya kusema hivi karibuni atazungumzia mustakabali wake ndani ya klabu hiyo.

Kwa nini asingesubiri sherehe za ushindi zipite, sababu ni moja tu, hakuwa sehemu ya taji hilo siku ya fainali, licha ya kucheza mchezo huo, kibaya zaidi ni Gareth Bale, ndiye aliyekuwa mwanamume midomoni mwa mashabiki wa soka.

Mbili, hakuna utofauti na nilichokizungumza hapo juu, kipindi hiki ambacho mkataba wake unakaribia ukingoni anajaribu kutingisha kibiriti aone kitatokea nini.

Amekuwa na msimu mzuri, licha ya kuanza kwa kusuasua, lakini alionyesha uwezo mkubwa sana na kuibeba timu hiyo pale alipohitajika kufanya hivyo.

Kauli yake ukiiangalia kwa ndani zaidi, utaipeleka kibiashara zaidi, hahitaji kingine zaidi ya kupata dau nono la mshahara.

Bale hawezi kuitetemesha sura ya Florentino Perez, inawezekana kauli ya Ronaldo ikamuacha na mawazo mengi kigogo huyo wa Real Madrid.

Ronaldo ni Real Madrid, licha ya Bale kufunga na kuwa stori kubwa katika fainali ile dhidi ya Liverpool, lakini stori yake ilisahaulika sekunde tu baada ya staa huyo wa Ureno kuongea.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*