googleAds

BADO UNAHITAJI KUJUA UMRI WA IBRAHIMOVIC?

NA OSCAR OSCAR

NI vigumu sana kuujua umri wa Zlatan Ibrahimovic, hasa katika kipindi hiki anachovaa jezi ya Manchester United. Unaijui sababu? Ni rahisi tu. Mchezaji anayetimiza majukumu yake uwanjani, mashabiki huwa hawana muda na maisha yake binafsi.

Habari za Ibra ana watoto wangapi, anatumia gari aina gani, haziwahusu mashabiki wa Manchester United kwa sasa. Hakuna anayetaka kujua kwa sababu umri wa Zlatan kwa sasa hauna maana yoyote. Watu wanahitaji zaidi magoli kuliko mambo yake binafsi.

Ukiutafuta umri halisi wa Ibrahimovic, unaweza kujichanganya mwenyewe kwa sababu anafunga sana kuliko umri wake. Ibrahimovic anaweza kuwa na deni kwa mashabiki wa timu hiyo pendwa zaidi duniani kwa sababu Manchester United wanahitaji kushinda kikombe msimu huu.

Ibra bado atakuwa na deni kwa mashabiki kwa sababu United wanahitaji kumaliza ndani ya nne bora msimu huu, lakini kuhusu uzee hakuna anayeuzungumzia na hakuna anayetaka kujua tena.

Jose Mourinho akiwa Inter Millan alimkuta Javier Zanetti, akiwa na umri wa miaka 37, lakini aliendelea kumtumia kama kijana mwenye umri wa miaka 22. Ibrahimovic ana miaka 35, lakini ukimtazama vizuri, bado anashabaha kama kijana wa miaka 22.

Bado analijua goli kama kijana mwenye njaa ya mafanikio. Bado unahitaji kujua umri wa Zlatan? Usipate tabu, fanya kujisogeza karibu na TV yako mwishoni mwa wiki hii.

Inawezekana kwamba, Ibra amepungua kasi lakini shabaha bado iko pale pale. Ndiyo maana ameshafunga mabao 16 msimu huu kwenye michuano yote wakati anayemfuatia ni Juan Mata mwenyewe mabao matano sambamba na Paul Pogba.

Bado unataka kujua umri wa Zlatan Ibrahimovic? Usikose kutazama mechi ya United ndani ya Old Trafford dhidi ya Sunderland boxing day. Ubora wake unawafanya watu wasahau habari za umri.

Utu uzima dawa ndani ya Manchester United, Zlatan Ibrahimovic na Michael Carrick, wamekuwa wachezaji muhimu sana msimu huu. United haijapoteza mchezo wowote ikiwa na Michael Carrick kwenye kikosi cha kwanza. Tayari Michael Carrick ameshinda mechi 10 na sare mbili kwenye kila mechi aliyoanza ndani ya kikosi cha United.

Carrick anafanya Paul Pogba azidi kuimarika kila kukicha, ni kwa sababu anamfanya awe huru zaidi. Kuna mtu anataka kufahamu umri wa Michael Carrick? Bila shaka hakuna hata mmoja na wengi wanatamani United imwongeze mkataba mwingine.

Ni kweli umri una mantiki kubwa kwa maisha ya mwanasoka lakini hawa ni wachezaji ambao unafurahia zaidi kiwango chao bila hata kujali umri wao. Hata kama wana miaka 80, bado ni aina ya wachezaji wanaohitajika zaidi ndani ya Manchester United. Umri wakati mwingine ni namba tu, kama ubora uko pale pale.

Baada ya kushinda mechi tatu mfululizo, kwa sasa unaweza kuanza kuiona United imara. United yenye ushindani na timu yenye uwezo wa kufanya chochote. Ni bora ukakimbizwa na Arsenal au Liverpool lakini si United. Hii ni timu ambayo wachezaji wake wanawaza kuitumikia zaidi klabu kuliko mafanikio yao binafsi.

Ni kweli miaka mitatu iliyopita wameyumba lakini uwepo wa kocha Jose Mourinho, kiungo Michael Carrick na mshambuliaji, Zlatan Ibrahimovic, kunaleta kitu cha tofauti. United ya Mourinho taratibu inaanza kupata uelekeo, taratibu inazidi kurejea njia kuu.

Wakati mwingine umri ni namba tu, uwezo wa mchezaji uwanjani ndiyo kila kitu. Bado unahitaji kujua umri wa Ibra? Endelea kufuatilia mechi za Manchester United, kuna siku utajua umri wa Zlatan Ibrahimovic. Watu wenye umri mkubwa ndiyo wanaoibeba Manchester United msimu huu, kama umejikita kwenye umri wa vyeti msimu huu, imekula kwako, Ibra hakamatiki.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*