Baada ya kutwaa taji jipya Ulaya, Ronaldo awaza kutetea Euro 2020

LISBON, Ureno

STAA wa timu ya taifa ya Ureno, anayekipiga Juventus ya Italia, Cristiano Ronaldo, amedai watalitetea taji la Kombe la Ulaya maarufu Kombe la Euro wakati fainali hizo zitakapofanyika mwakani Uwanja wa Wembley, England.

Ureno walibeba taji la Euro ya mwaka 2016 baada ya kuwafunga Ufaransa bao 1-0 ambao walikuwa wenyeji wa michuano hiyo.

Kauli hiyo ya Ronaldo ilikuja baada ya juzi kuichapa Uholanzi bao 1-0 na kunyakuwa taji la Ligi ya Mataifa Ulaya ambayo ni mashindano mapya yaliyoanzishwa na Chama cha Soka cha Ulaya (UEFA).

Nyota huyo alifunga ‘hat-trick’ katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Uswisi ambapo Ureno ilishinda mabao 3-1 na kufuzu fainali.

Licha ya umri wake wa miaka 34, Ronaldo alisisitiza atakuwepo katika kikosi cha Ureno ambacho kinapambana kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Euro mwakani.

“Nataka kuwa sehemu ya mafanikio na timu hii, najisikia vizuri sana. Kikosi chetu kina wachezaji vijana na ninaimani tutalitetea taji la Euro, lengo langu ni kuisaidia taifa langu kufika malengo haya,” alisema Ronaldo.

Mwanasoka huyo ameifungia Ureno mabao 88 katika mechi 158, na kumfanya kuingia kwenye historia ya mchezaji aliyefunga mabao mengi katika mechi za kimataifa Ulaya.

Ureno chini ya kocha mkuu, Fernando Santos, imepata mafanikio kwa ngazi ya kimataifa licha ya kikosi chao kupondwa na baadhi ya wachambuzi wa soka.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*