AZAM MABINGWA WA KIHISTORIA

 

NA MWANDISHI WETU


 

IMG_0844

AZAM FC wamefanikiwa kunyakua ubingwa wa Kombe la Mapinduzi mwaka huu kwa mara ya nne, baada ya kuwafunga URA ya Uganda kwa penalti 4-3 katika mchezo wa fainali uliopigwa juzi usiku kwenye Uwanja wa Amaan, Visiwani Zanzibar.

Kwa ubingwa huo, Azam wamekuwa mabingwa wa kihistoria kwa kuchukua taji hilo la Mapinduzi kwa mara nne na kuwazidi Simba ambao wao walikuwa wakilingana nao kwa kuwa mabingwa mara tatu.

Pamoja na kuweka rekodi ya kuchukua taji hilo mara nne, pia Azam wameweza kuchukua taji hilo mara mbili mfululizo kwa mara ya pili, ambapo mara ya kwanza walilichukua mwaka 2012 na 2013 kabla ya kuchukua tena mwaka jana na mwaka huu.

Kwa mara ya kwanza Azam walitwaa ubingwa huo mwaka 2012 kwa kuwafunga Jamhuri mabao 3-1, kabla ya kutetea taji hilo mwaka uliofuata kwa kuifunga Tusker mabao 2-1.

Bao la ushindi katika fainali ya mwaka 2013 lilifungwa na Gaudance Mwaikimba, baada ya Tusker kupata bao la kuongoza kupitia Jese Were na beki wa Azam, Jockins Atudo, kusawazisha kwa penalti baada ya Mwaikimba kuchezewa vibaya na mwamuzi Ramadhani Kibo kuamuru iwe penalti.

Dakika 90 za fainali hiyo zilimalizika kwa sare 1-1 na kuongozwa dakika 30 na Mwaikimba kufunga bao hilo dakika ya 92 na kuipa ubingwa akiwa amefunga mabao mawili kwenye michuano hiyo huku Atudo akifunga manne.

Baada ya taji hilo kuchukuliwa na KCCA mwaka 2014, Simba (2015) na URA (2016), Azam walilibeba tena mwaka jana kwa kuwafunga Simba bao 1-0, bao hilo likifungwa na Himid Mao Mkami dakika ya 12 kwa shuti kali umbali wa takribani mita 25 baada ya kupokea pasi ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na kusogea hatua chache na kuachia mkwaju huo.

Mwaka huu Azam wameanza michuano hiyo wakiwa Kundi A, pamoja na Simba, URA, Mwenge na Jamhuri, ambapo katika mechi ya kwanza iliyochezwa Desemba 31, mwaka huu, Azam waliifunga Mwenge mabao mawili ambayo yote yalifungwa na Paul ‘Pogba’ Peter.

Mchezo wao wa pili ulikuwa dhidi ya Jamhuri na kuwafunga mabao 4-0, ambayo yalifungwa na Bernard Athur, Salimin Hozza, Yahaya Zayd na Paul ‘Pogba’, kabla ya kuchapwa bao 1-0 dhidi ya URA ya Uganda na kuifunga Simba bao 1-0 lililowekwa nyavuni na Idd Kipagwile ‘Mtoto Idd’.

Azam walitinga nusu fainali na kucheza na Singida United ambao waliwachapa bao 1-0, ambalo lilifungwa na Shaban Idd ‘Chilunda’ na kutinga fainali dhidi ya URA, ambao waliwatoa Yanga kwenye mchezo wa nusu fainali kwa matuta 5-4.

Fainali hiyo iliamuliwa kwa matuta baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 za mchezo huo uliokuwa mkali na wa kipekee bila ya kufungana, ambapo penalti za Azam zilifungwa na nahodha Himid Mao ‘Ninja’, Yakubu Mohammed na winga Enock Atta, huku beki wa kushoto, Bruce Kangwa akikosa, lakini Agrey Morris aliifungia timu yake tuta la ushindi baada ya wachezaji wa wapinzani wao kukosa penalti mbili zilizodakwa na Razak Abalora.

Hili ni taji la kwanza la kocha Aristica Cioaba, ambaye ndio kocha wa pili nchini Romania mwenye leseni A ya Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) tangu atue Azam mwaka.

 

Timu nyingine zilizochukua taji hilo

2007-Yanga

2008-Simba

2009-Miembeni

2010-Mtibwa

2011-Simba

2012-Azam

2013-Azam

2014-KCCA

2015-Simba

2016-URA

2017-Azam

 

 

 

 

 

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*