AZAM KUSAKA POINTI TISA KANDA YA ZIWA

NA SALMA MPELI


KIKOSI cha Azam FC, kimeanza mazoezi yake jana kwa ajili ya kujiweka sawa na mechi tatu zijazo za Ligi Kuu Tanzania Bara itakazocheza ugenini Kanda ya Ziwa dhidi ya Mwadui ya Shinyanga (Septemba 14), Biashara United ya Mara (Septemba 19) na Alliance ya Mwanza, Septemba 23.

Akizungumza na BINGWA jana, Kocha Msaidizi wa Azam, Idd Nassoro ‘Cheche’, alisema wameanza mazoezi kwa ajili ya kuhakikisha wanarejea na pointi tisa katika mechi hizo tatu zilizo mbele yao.

“Tunaingia kambini leo (jana) na kuanza mazoezi kwa ajili ya maandalizi yetu ya mechi tatu zijazo ugenini, tumejipanga kuhakikisha tunapata pointi zote tisa katika mechi hizo ili kujiweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo,” alisema Cheche.

Katika hatua nyingine, timu hiyo juzi asubuhi ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Reha FC inayoshiriki Ligi Daraja la Pili katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Akizungumza na BINGWA jana, Ofisa Habari wa Azam, Jafari Idd, alisema katika mchezo huo, mabao yao yalifungwa na Wazir Junior aliyefunga la kwanza akitumia uzembe wa mabeki likiwa ni la kusawazisha kwa timu yake, huku Danny Lyanga, akifunga bao la pili.

Alisema Reha walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia mshambuliaji wao, Maliki Dachi, ambaye ndiye mfungaji wa mabao yote mawili kwa timu yake, moja katika kila kipindi.

Mchezo huo ni wa tatu wa kirafiki kwa Azam kwa muda huu wakati Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) ikiwa imesimama kupisha mechi za timu za Taifa za kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwakani nchini Cameroon.

Mechi za awali za kirafiki kwa Azam, ilipoteza mmoja dhidi ya Transit Camp kwa mabao 2-1, huku ikitoka suluhu na Arusha United (zamani Oljoro JKT), ambayo mwezi ujao itaanza harakati za kupambana kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*