AZAM KUMKOSA KUTINYU MECHI NA MWADUI

 |  NA WINFRIDA MTOI  


 

TIMU ya Azam FC itamkosa kiungo wao Mzimbabwe, Tafadzwa Kutinyu, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mwadui FC, unaotarajiwa kupigwa kesho kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.

Kutinyu anatarajia kuwasili leo jijini Dar es Salaam, akitokea Congo Brazzaville, ambako alikuwa na timu ya Taifa ya Zimbabwe, iliyocheza mechi ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa (Afcon) nchini humo.

Akizungumza na BINGWA jana, Meneja wa Azam FC, Phillip Allando, alisema Kutinyu atakapowasili Dar es Salaam atapanda ndege nyingine ya kwenda Mwanza, kisha kupanda basi ili kuungana na timu Shinyanga.

Alisema mchezaji huyo kwa muda mrefu hakuwa na timu, hivyo itakuwa ni ngumu kuwepo kwenye kikosi kitakachoivaa Mwadui  kesho.

“Wachezaji waliokuwa katika majukumu ya timu zao za taifa wamerejea, isipokuwa Kutinyu anakuja kesho (leo), atashukia Dar es Salaam na moja kwa moja ataunganisha ndege nyingine hadi Mwanza na kupanda basi kwenda Shinyanga,” alisema Allando.

Aliwataja wachezaji waliokuwa timu za taifa kuwa ni Nicolas Wadada (Uganda), Yahya Zaid, David Mwantika, Frank Domayo, Aggrey Morris na Mudathir Yahya (Taifa Stars).


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*