Aussems:Uzoefu kimataifa kuipa ubingwa Simba

*Adai mwendo wa pointi tatu unaanzia kwa Coastal Union kesho

OSCAR ASSENGA, TANGA

KOCHA wa timu ya Simba, Patrick Aussems, ametamba kuwa kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wamepata uzoefu mkubwa na sasa mpango wao ni kusaka pointi tatu kila mechi kuanzia mchezo wao wa kesho dhidi ya Coastal Union.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Popatlal mjini Tanga, Aussems, alisema wamepata uzoefu mkubwa kwenye mechi hizo.

Simba walitolewa na TP Mazembe mjini Lubumbashi nchini DR Congo kwa kuchapwa mabao 4-1, katika mchezo wa pili wa robo fainali baada ya ule wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kumalizika kwa sare ya 0-0, ambapo Aussems amekataa kuwalinganisha Wekundu hao wa Msimbazi na wapinzani wake hao akisema wana uzoefu mkubwa kuliko wao.

Aussems amesema walifanikiwa kupata bao dakika za mwanzoni, lakini walijitahidi kuzuia ila walishindwa lakini wanashukuru wameweza kujifunza kwa kuwa mechi hiyo ya mwishoni mwa wiki ilikuwa tofauti na ile waliyocheza nchini Misri.

“Ukilinganisha Mazembe na Simba, Mazembe wana uzoefu mkubwa, lakini msisahau kwamba mpango wetu ulikuwa ni kufika hatua ya makundi lakini tumeenda mpaka robo tukafungwa, lakini sasa tunaelekeza akili zetu kwenye ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara,” alisema Aussems.

Akizungumzia mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika kabla hawajatolewa, Aussems, anasema kwa mechi hizo sita ama saba walizocheza na kutolewa na TP Mazembe, zimewapa wachezaji wake uzoefu wa miaka miwili.

“Tumejifunza mambo mengi, mfano wa mechi tuliyocheza Jumamosi na TP Mazembe. Mechi kama hizi za Ligi ya Mabingwa Afrika zinakupa uzoefu mkubwa,” alisema Aussems.

“Hivyo mechi sita au saba tulizocheza ni sawa tumecheza mechi 15 za Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo ni muhimu kwa wachezaji na naweza kusema zimewapa wachezaji uzoefu wa miaka miwili,” aliongeza kocha huyo.

Kocha huyo anasema baada ya kutolewa sasa wamerejea kwenye ligi na mpango wao ni kukusanya pointi tatu katika kila mechi ili kubeba ubingwa haraka iwezekanavyo.

“Kwa sasa naweza kusema tumerejea kweye ligi na tuna mpango wa kubeba pointi tatu kila mechi ili kuweza kubeba ubingwa kwa mara nyingine tena,” alisema Aussems.

Simba watakuwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani kuvaana na wenyeji wao Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kesho saa 10:00 jioni.

Katika mchezo huo, Simba watawakosa wachezaji wao watatu ambao ni beki, Pascal Wawa, aliyeumia katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe uliochezwa wiki iliyopita Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Wengine ni beki, Jjuuko Murshid na kiungo mkabaji, James Kotei, ambao wote walipata majeraha katika mchezo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe mjini Lubumbashi.

Simba wako nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na pointi 57 baada ya kushinda mechi 18 na kutoka sare tatu na kupoteza mmoja kati ya michezo 22.

Huku wenyeji wao Coastal Union wanashika nafasi ya nane baada ya kucheza mechi 32 wakishinda tisa na kutoka sare 14 wakifungwa tisa.

Hivyo mchezo huo ni muhimu kwa timu zote mbili, ambapo Simba wanataka kutetea taji lao wakati Wagosi wa Kaya wanataka kujihakikishia nafasi ya kutoshuka daraja baada ya kupanda msimu uliopita.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*