Aussems: Hata tucheze asubuhi, pointi tatu lazima

NA MWAMVITA MTANDA

KOCHA wa Simba, Patrick Aussems, amesema pamoja na kubanwa na ratiba ya ligi kwa kucheza mechi kila baada ya siku tatu kufidia viporo vyao na kupangiwa kucheza mchana baadhi ya mechi, ameahidi kutoa dozi hata kama watacheza asubuhi.

Simba, ambao wameibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Costal Union juzi Jumatano kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, watakuwa na mechi nyingine kesho mjini Bukoba.

Lakini kocha wa timu hiyo ya Wekundu wa Msimbazi, ambayo itaondoka leo kuelekea Kanda ya Ziwa kwa ajili ya mchezo huo na Kagera Sugar, amesema ratiba imekuwa ngumu na ya kuchosha wachezaji wake, lakini bado wataendelea kutoa dozi kwa wapinzani wao.

“Tumetoka katika kibarua kigumu cha michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tumekuja kwenye kazi ngumu ya kutetea ubingwa wetu,” alisema Aussems.

Pia kocha huyo aliiponda Bodi ya Ligi, akisema hali hiyo inatokana na mpangilio mbovu wa bodi hiyo kwa kushindwa kupanga vizuri ratiba hiyo iendane na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Bodi ya Ligi walikuwa na uwezo wa kupanga ratiba kuendana na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ila wenyewe wameshindwa kufanya hivyo,” alisema Aussems.

Akizungumzia suala la kutetea ubingwa wa Ligi Kuu, Aussems alisema:

“Kuchukua ubingwa si jambo la kuzungumza kwa mdomo, bali linahitaji matendo yenye uthubutu, ikiwa ni pamoja na mipango yake ndani ya kikosi.

“Ni rahisi kusema nitashinda, lakini ni rahisi pia kupoteza, japokuwa tumebaki na mechi nyingi, ila kila timu inahitaji ushindi, ndiyo maana kwa sasa nimewekeza mawazo yangu zaidi kwenye Ligi Kuu na kuwanoa wachezaji kwa bidii,” alisema Aussems.

Aussems alisema hata kama mechi zilizobaki zitaendelea kuchezwa saa 8:00 mchana, atafanya jitihada kubwa kuwajenga wachezaji wake kisaikolojia ili kuizoea hali hiyo.

Alisema kutokana na mfumo wa soka la Tanzania, timu nyingi zimezoea kucheza mechi saa 10:00 jioni, jambo ambalo linaweza kuiathiri Simba kama hawatakuwa umakini.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*