googleAds

AUSSEMS AVUJISHA USAJILINA

MWAMVITA MTANDA

WAKATI wapenzi wa Simba wakiendelea kusikilizia majina ya wachezaji wao waliosajiliwa kuitumikia timu yao msimu ujao, Kocha Mkuu wa Wekundu wa Msimbazi hao, Patrick Aussems, ameweka wazi nyota anaowataka watakaomwezesha kufanya makubwa zaidi.

Baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu tangu kumalizika kwa msimu uliopita, hatimaye uongozi wa Simba umeanza kuanika picha za wachezaji waliomalizana nao, hadi sasa wengi wakiwa ni wale waliokuwa nao kikosini.

Kati ya wachezaji watano ambao hadi sasa wameanikwa na klabu hiyo kusaini mikataba, ni mmoja tu ambaye hakuwamo katika kikosi cha msimu uliopita, kipa Benno Kakolanya aliyejiengua Yanga kutokana na madai ya mshahara na dau la usajili.

Wengine ni kipa Aishi Manula, Erasto Nyoni, Jonas Mkude na John Bocco ambao walimaliza mikataba yao, huku wengine zaidi wakiendelea kuwekwa hadharani kadri siku zinavyokwenda.

Tayari uongozi wa Simba kupitia Ofisa Mtendaji Mkuu wao, Crescentius Magori, umetangaza kuanza kushusha vifaa vya kigeni wiki ijayo.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dar es Salaam, Magori alisema: “Wachezaji wote wazawa waliokuwa wamemaliza mikataba na tunahitaji kuendelea nao, tumemalizana, kuanzia kesho (jana), itaanza patashika ya wachezaji wa kimataifa ambao watakuwa bora kuliko wale waliopita.

“Tunasajili wachezaji wa kimataifa wanaoweza kututoa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wapo  wachezaji wengi kutoka mataifa mbalimbali wanakuja kuomba kuchezea, lakini tunawachunguza.”

Lakini wakati Magori akiendelea kuwapa wapenzi wa soka kitendawili kilichokosa majibu, Aussems ambaye yupo nchini kwao Ubelgiji kwa mapumziko, ameliambia BINGWA jana kuwa wachezaji wa kigeni watakaotua Simba, wana kiwango cha juu zaidi ya wakali wake, Meddie Kagere na John Bocco.

“Unataka majina? Subiri kwanza, sipendi kuuingilia uongozi kwani unaendelea na majukumu yao. Ila fahamu tu kwamba tunaleta wachezaji wenye kiwango cha juu, hakuna hata mmoja wa kubahatisha,” alisema.

Alisema kuwa kabla ya kuondoka nchini, aliwaagiza viongozi wa Simba kuwaongezea mikataba baadhi ya  nyota wake wa kutumainiwa, wakiwamo Nyoni, Mkude  na Bocco.

“Kikosi changu kina wachezaji wazuri na wenye uwezo mkubwa, lakini hawa wachezaji (akina Nyoni), niliwahitaji sana, naweza kusema ni muhimili wa timu,” alisema Aussems.

Aliwataka wapenzi wa Simba kutokuwa na wasiwasi juu ya usajili wa timu yao kwani kila kitu kimeshakamilika, imebaki kuwashusha tu hapa nchini.

Msimu uliopita ulikuwa wa mafanikio makubwa kwa Aussems baada ya kuifikisha timu hiyo hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku pia ikitetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*