googleAds

AUSSEMS ATOA KAULI TATA

NA MWAMVITA MTANDA

KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, ametoa kauli tata ambayo huenda ikawachanganya wapenzi wa klabu hiyo juu ya majaliwa yake ndani ya Wekundu wa Msimbazi hao.

Aussems raia wa Ubelgiji, alijizolea umaarufu mkubwa ndani ya Simba baada ya kuiwezesha timu hiyo kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini pia kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.

Mafanikio hayo, yalionekana kuwapandisha mzuka wapenzi wa Simba na hata viongozi wao na hivyo kuweka mikakati ya kufanya makubwa zaidi msimu huu.

Katika hilo, Wekundu wa Msimbazi hao walifanya usajili waliouita ‘bab kubwa’, huku shabaha yao kubwa ikiwa ni kufika mbali zaidi Ligi ya Mabingwa Afrika kuiliko ilivyokuwa msimu uliopita.

Kuhakikisha lengo lao hilo linatimia, uongozi wa Simba ulitupa macho huku na huko kusaka wachezaji na kunasa vifaa kutoka nchi za Brazil, Sudan, Kenya, DR Congo na wazawa kadhaa waliotamba msimu uliopita.

Lakini kwa bahati mbaya, mambo yamekwenda tofauti na matarajio yao baada ya kikosi chao kutolewa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali na sasa wakibakiwa na kibarua cha kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Bara pekee.

Wakati wapenzi wa Simba wakisubiri kuona nini kitaendelea ndani ya kikosi chao, hasa baada ya kuanza Ligi Kuu Bara kwa ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya JKT Tanzania, Aussems ameibua jipya akisema hajui hatma yake Msimbazi.

Kocha huyo aliyasema hayo alipozungumza na BINGWA jana kutaka maoni yake juu kiwango kilichoonyeshwa na Taifa Stars pamoja na wachezaji wake dhidi ya Burundi mwishoni mwa wiki iliyopita, akiwamo kipa Juma Kaseja.

“Taifa Stars ilicheza vizuri sana na hakika ilistahili kushinda na kuingia makundi.

“Kuhusu wachezaji, kila mmoja alicheza katika kiwango cha juu…najivunia wachezaji wangu (wa Simba), nao walicheza vizuri sana.

“Natamani sana kudumu ndani ya hii timu (Simba) ili nkiendelee kuwatengeneza wachezaji wangu, lakini siwezi kusema kwa maneno peke yake bali nahitaji nifanye kazi kubwa zaidi ili waendelee kuniamini.

“Lakini mimi ni mwajiriwa kama ilivyo kwa hawa wachezaji, siwezi kujua nini kitatokea juu ya majaliwa yangu ndani ya Simba siku zijazo,” alisema.

Aussems alisema pamoja na hilo, anaendelea kukinoa kikosi chake kiweze kufanya vema katika mechi zao zijazo za Ligi Kuu Bara, huku azma yake kubwa ikiwa ni kufunga mabao mengi kila watakaposhuka dimbani.

Mchezo ujao wa Simba wa Ligi Kuu Bara utakuwa dhidi ya Mtibwa Sugar, ukipigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*