googleAds

Aussems ataka pointi 15 tu mechi tano Dar

MAREGES NYAMAKA NA GLORY MLAY

KOCHA wa Simba, Patrick Aussems, ameshaanza kupigia hesabu ubingwa wa Ligi Kuu Bara huku akihitaji ushindi katika mechi tano kati ya nane walizobakisha.

Mbeligiji huo juzi alikiongoza kikosi chake hicho kuibuka na ushindi muhimu wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Bao pekee katika mchezo huo lililowafanya Wekundu wa Msimbazi kufikisha pointi 78 lilifungwa na Emmanuel Okwi dakika ya 11 kwa guu la kulia akitumia vyema pasi ndefu ya kiungi James Kotei.

Ni ushindi ambao uliwafanya kusalia katika nafasi ya pili lakini kupunguza pengo la pointi na watani zao wa jadi, Yanga, ambao wanaongoza ligi wakiwa na pointi 80.

Baada ya mechi hiyo, Aussems alieleza furaha yake kuvuna pointi sita huku awali akiwa alishacheza na Mbeya City na kushinda mabao 2-1.

“Tulicheza (dhidi ya Tanzania Prisons) kwa kujilinda zaidi hususan kipindi cha pili, lakini kikubwa ni ushindi tulioupata, pointi zote sita tumechukua katika michezo yote miwili migumu.

“Tunarejea nyumbani kucheza mechi tano ambazo tunahitaji pointi zote tukianza na Coastal Union Jumatano (kesho), “alisema Mbelgiji huyo.

Michezo mitano ya karibu ambayo inawakabili Wekundu hao Msimbazi ni dhidi ya Coastal Union, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Azam na Ndanda.

Endapo Simba itashinda mechi hizo zote tano, itakuwa imefikisha pointi 93 ambazo zitawasaidia kutetea taji la Ligi Kuu Bara huku wakiwa bado na mechi tatu mkononi.

Idadi hiyo ya pointi haziwezi kufikiwa na timu yeyote ikiwemo Yanga ambao kama wakishida mechi zote zilizosalia wanafikisha pointi 92.

Wakati huo huo, nahodha wa timu ya Coastal Union, Hussein Sharif ‘Casillas’, amesema shauku yao kubwa ni kuwafunga mabingwa watetezi Simba, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, utakaochezwa kesho Dar es Salaam.

Akizungumza na BINGWA jana, Casillas alisema wapinzani wao hao ni timu nzuri, lakini wanapocheza nao lazima wajipange vyema kuhakikisha wanaweka ulizi wa kutosha na kufanya mashabulizi ya kushutukiza ili waweze kupata ushindi.

Alisema kila mchezaji amepewa jukumu lake uwanjani lengo likiwa ni kutopoteza mchezo huo ili kuzidi kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

“Simba wanawachezaji wazuri hususan safu ya ukabaji jambo ambalo tulilishuhudia tulipocheza nao Mkwakwani na wakatufunga ila tumetambua mapungufu yao na tutayatumia ili tuondoke na pointi tatu,” alisema.

Coastal Union wanashika nafasi ya 10 baada ya kujikusanyia pointi 41 kutokana na michezo 33 ambapo wameshinda tisa, kutoka sare 14 na kufungwa 19.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*