Aussems asema dunia sasa inaijua Simba, Tanzania mashabiki wajivunie timu yao

NA MWANDISHI WETU

KOCHA wa Wekundu wa Msimbazi, Simba, Patrick Aussems, ameweka wazi kuwa kwa sasa dunia inajua Simba na Tanzania ilipo, kutokana na hatua nzuri iliyopiga katika soka, hivyo kumtaka kila shabiki wa timu hiyo kujivunia hatua waliyofikia.

Aussems aliandika hayo katika ukurasa wake wa kijamii wa twitter, mara baada ya kuondolewa na TP Mazembe katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 4-1.

Kocha huyo Mbelgiji alieleza anaishukuru Simba na mashabiki wake, walioisapoti timu hiyo mpaka kufikia hatua hiyo, ambayo walivuka malengo.

Awali Simba ilikuwa imepanga kuhakikisha inaingia hatua ya makundi, lakini ikavuka malengo kwa kucheza robo fainali ambayo ni hatua kubwa kwao.

“Tutarudi kwenye michuano hii mwakani tukiwa wazuri zaidi, sasa hivi tutahakikisha sisi na mashabiki wetu tunachukua ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara nyingine,” alisema.

Hata hivyo, Mbelgiji huyo mara kadhaa amekuwa akivutiwa na mashabiki wao, ambao wamekuwa pamoja katika kila hatua, hali ambayo anaamini wamechangia kwa kiasi kikubwa kwa wao kutinga robo fainali.

Katika hatua ya makundi, mashabiki hao walikuwa wakiujaza Uwanja wa Taifa, wenye uwezo wa kubeba watu 60,000, hali iliyoufanya kuwa kaburi la kila mgeni aliyekanyaga ardhi ya Tanzania.

BINGWA lilipomtafuta kuzungumza naye alisema mwisho wa safari yao katika michuano hiyo, ndio mwanzo wa kujipanga upya kuelekea msimu ujao, ambapo kwa sasa akili zao inabidi wazihamishie katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Tumehitimisha safari yetu kwenye Ligi ya Mabingwa, lakini vita iliyo mbele sasa ni kutetea ubingwa wetu kwenye Ligi ili kuwapoza mashabiki wetu,” alisema.

Alisema wamerejea nchini wakiwa na kazi moja tu, kutetea ubingwa wao na kujipanga na michuano mingine iliyo mbele yao.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*