AUSSEMS ALETEWE MSAIDIZI ATAKAYEFANYA NAYE KAZI

WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara ikiendelea katika mzunguko wa nane, Simba wamevunja mkataba na kocha wake msaidizi, Masoud Djuma.

Simba walifikia hatua hiyo baada ya kujiridhisha kuwa katika benchi la ufundi kulikuwa hakuna maelewano kati ya Djuma na kocha mkuu, Patrick Aussems, hivyo kukosekana kwa ufanisi ndani ya timu hiyo.

Kutokana na sababu hiyo, timu ya  Simba ilijikuta ikishindwa kufanya vizuri katika michezo mitatu ya ligi hiyo baada ya kutoka sare miwili na kupoteza mmoja.

Matokeo ya timu ya Simba kwa kiasi kikubwa yalisababishwa na kutokuwa na ushirikiano katika benchi la ufundi.

BINGWA tunasema kwa kuwapo kwa tofauti za makocha mawili wa Simba, Djuma na Aussems kulitoa nafasi kwa wapinzani wao kuweza kufanya vizuri katika michezo ambayo wamecheza.

Tunasema mafanikio yoyote katika timu yanachangiwa na ushirikiano wa pamoja wa makocha, wachezaji, viongozi na  mashabiki, kitendo cha Djuma na Aussems kutoiva chungu kimoja kingeweza kuathiri zaidi matokeo ya michezo yao.

Kwa upande wetu, tunasema pamoja na Simba kuchukua uamuzi wa kuvunja mkataba wa Djuma, lakini bado wanajukumu kubwa la kuhakikisha wanamleta msaidizi wa Aussems ambaye hatavuruga tena benchi la ufundi la timu hiyo.

BINGWA tunasema kwamba, Simba wanatakiwa kuwa makini katika suala la kumleta kocha msaidizi ambaye hatavurugana na Aussems kama wanahitaji kutimiza malengo yao waliyojiwekea kwa msimu huu.

Tunaamini kwamba kuna makocha wengi wakiwamo wazawa ambao wanaweza kufanya kazi kwa karibu na Aussems na Simba kuweza kupata mafanikio katika michuano ya ndani na kimataifa.

Hivyo basi, ni jukumu la viongozi wa Simba kutuliza akili na kumleta kocha msaidizi ambaye atakuwa tayari kufanya kazi na safu nzima ya benchi la ufundi la timu hiyo.

BINGWA tunaamini kwamba, mvurugano uliotokea hivi sasa katika benchi la ufundi la timu hiyo, viongozi wa Simba watakuwa wamepata funzo, hivyo tunadhani hawatarudia kosa kwa kumwajiri kocha aina ya Djuma.

Tunasisitiza kwamba, Simba wanatakiwa kumleta msaidizi wa Aussems ambaye ataleta ushirikiano kwenye benchi la ufundi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*