googleAds

ANTHONY JOSHUA

LONDON, England

*Mkimbizi wa Nigeria anayewaliza wazungu ulingoni

*Akataliwa Nigeria, aiwakilisha England

JINA la Anthony Joshua limezidi kuwa maarufu baada ya juzi kumpiga kwa ‘knockout’ KO, bondia mtata wa Urusi, Alexander Povetkin, katika pambano lililofanyika Uwanja wa Wembley.

Ameshika vichwa vya habari duniani kote kutokana na uwezo mkubwa wa kutupa makonde kwa wapinzani wake ambao wote amewachapa.

Bondia huyo raia wa England, amefanikiwa kucheza mapambano 22 huku akishinda yote, mchanganuo wa mapambano 21 kwa KO na moja kwa pointi.

Tayari anamiliki mikanda ya IBF, WBO na WBA huku akiutolea macho mkanda wa WBC ambao upo mikononi mwa Deontay Wilder raia wa Marekani.

Mashabiki wa masumbwi wanatarajia siku moja kuona pambano la wakali hao ambao wanatambiana tu katika vyombo vya habari kwa ubabe wanaouonyesha mbele ya wapinzani wao.

Huku Anthony akiyateka macho ya wapenzi wa masumbwi alipofanikiwa kumchapa Wladimir Klitschko kwa KO.

JOSHUA NI NANI?

Ni raia wa England mwenye asili ya Nigeria, alizaliwa Oktoba 15, 1989 jijini Watford katika Hospitali ya Hertfordshire.

Mzizi wa Nigeria upo kwa upande wa mama yake, Yeta Odusanya na baba yake, Robert Joshua ni raia wa England, lakini jina kamili la bondia huyo ni Anthony Oluwafemi Olaseni Joshua.

Maisha yake ya utotoni aliishi Nigeria, alipofikisha miaka saba alielekea England na familia yake ambako alijiunga na Shule ya Sekondari ya Kings Langley.

Anthony alikuwa anapenda michezo na mchezo wa soka aliupenda sana enzi za utoto wake, ukiacha hilo, alipokuwa na miaka tisa alivunja rekodi kwa kukimbia mita 100 kwa sekunde 11.6 wakati yupo shule.

Huku rafiki yake wa karibu, Martin Anderson, akishikwa na butwaa kubwa kumwona Anthony akiwa bondia wakati alikuwa na ndoto za kuwa mchezaji wa mpira wa miguu wa kulipwa.

SAFARI YA UBONDIA

Kabla ya kuwa bondia wa kulipwa na maarufu, Anthony alifanya kazi katika kampuni moja ya ujenzi.

Jambo la kufurahisha zaidi aliwahi kumpiga mtu na kufungwa jela kwa miezi mitatu, wakati alipoachiwa alianza kufanya mazoezi ya ubondia.

Mwaka 2007 akiwa na miaka 18, alianza safari ya ubondia ukiwa ni ushauri wa binamu yake, Ben Ileyemi ambaye naye alikuwa bondia baadaye.

Alianza kujifua katika moja ya kituo cha Finchley ABC kilichopo London Kaskazini, ambacho pia kilimkuza bondia wa uzito wa juu, Dereck Chisora.

Mwaka 2009, alipigana na kushinda taji la Haringey Box Cup na kufanikiwa kulitetea taji hilo mwaka 2010 ambao pia alikuwa mshindi wa ABA Championship.

Aliwekewa kiasi cha pauni 50,000 mezani ili ajiunge na moja ya kituo nchini humo England, lakini alikataa huku akisisitiza hafanyi mchezo huo sababu ya fedha bali kwa mapenzi yake.

Mwaka 2010, alifanikiwa kujumuishwa katika timu ya Taifa ya Umoja wa Waingereza ‘Great Britian’ na baadaye aliendelea na kuwa mshindi wa Amateur Boxing Championship baada ya kumtwanga mpinzani wake, Amin Isa.

Mwaka uliofuata katika michuano hiyo alifanikiwa kumchakaza bondia hatari raia wa Romania, Mihai Nistor, akiweka rekodi ya pointi 40-3 ambayo haikuwahi kuwepo.

AKATALIWA NIGERIA

Mwaka 2008, Anthony alikataliwa na Chama cha Ngumi cha Nigeria alipohitaji kusainiwa aiwakilishe nchi hiyo katika michuano ya Olimpiki iliyofanyika Beijing, China.

Bondia huyo hafichi asili yake kuwa ni Mnigeria, mara kwa mara amekuwa akitamka na katika mkono wake mmoja amejichora mchoro wa ramani ya eneo mama yake anapotoka ambako panafahamika kwa jina la Yoruba.

Mmoja wa makocha waliomkataa, Obisia Nwankpa wakati ule alitoa sababu za wao kufanya hivyo, huku akijitetea kuwa bondia huyo alichelewa kujiunga na kambi.

“Tulimpa nafasi ya kufanya majarabio lakini hakutokea kwa muda tulioupanga, alikuja kuonekana siku ambayo tumemaliza maandalizi yetu ya kuelekea Beijing na kwa pamoja tuliamua kuachana naye,” alisema Obisia.

 

 

 

 

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*