ANAVIZIA………………… Unaambiwa Mourinho anasubiri simu ya Levy

LONDON, England

KWELI vita ya panzi ni furaha kwa kunguru. Hali ambayo ipo katika kikosi cha Tottenham hivi sasa, imekuwa ikimfurahisha Jose Mourinho ambaye anatajwa kufuatilia kwa ukaribu kazi ya ukocha ndani ya klabu hiyo.

Mourinho amekuwa nje ya kazi hiyo tangu alipofukuzwa na Manchester United Desemba mwaka jana, akikaribia kukamilisha mwaka bila kuwa na timu ya kufundisha ikiwa ni mara ya kwanza kwake.

Hata hivyo, imebainika kuwa Tottenham watakutana na upinzani mkali wa kumshwishi Mreno huyo ambaye anafukuziwa vikali na Real Madrid, ambao wanafikiria kumfukuza Zinedine Zidane.

Rais wa Real Madrid, Florentino Perez amekuwa na mahusiano mazuri na Mourinho ambaye alikiri kuwasiliana naye kila wakati.

Mourinho mwenye umri wa miaka 56, aliwahi kusema kuwa anasubiri wakati sahihi wa kufanya kazi hiyo, kwa sasa akiwa anafanya kazi ya uchambuzi wa soka katika kituo cha Sky Sports.

Kocha huyo aliyewahi kuzifundisha timu za FC Porto, Chelsea, Inter Milan, Real Madrid na Manchester United hivi karibuni alikataa ofa ya kuifundisha klabu yake ya zamani ya Benfica.

Pia, aliifungia vioo ofa ya pauni milioni 90 kutoka kwa tajiri wa klabu ya Guangzhou Evergrande inayoshiriki Ligi Kuu China.

“Inabidi niwe mpole na mvumilivu kwa sasa, nasubiri kazi sahihi, naamini itakuja, bado naamini hivyo, muda bado upo,” alisema Mourinho.

Hakuna kingine anachosubiri kocha huyo Mreno zaidi ya simu kutoka kwa Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy, kwa ajili ya kuinoa klabu hiyo yenye maskani yake Kaskazini mwa London.

Tottenham wamekuwa na mwanzo mbaya wa msimu huu chini ya Mauricio Pochettino, ingawa inadaiwa klabu hiyo haina mpango wa kumfukuza kocha huyo raia wa Argentina.

Pochettino alijiunga na Tottenham mwaka 2014 akitokea Southampton na mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2023, hata hivyo, kocha huyo anafukuziwa vikali na timu ya Manchester United.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*