AMUNIKE ASALIMU AMRI KWA NYONI, MKUDE

NA MWAMVITA MTANDA


 

KOCHA mkuu wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Emmanuel Amunike, amesema atawajumuisha kikosini mwake nyota kadhaa wa Simba, wakiwamo kiungo mkabaji, Jonas Mkude.

Mbali ya fundi huyo, wachezaji wengine aliowataja ni beki Erasto Nyoni na mshambuliaji, John Bocco.

Mnigeria huyo amefikia uamuzi huo kutokana na kile alichodai kubaini pengo la nyota huyo na wenzake kadhaa wakati Stars ilipomenyana na Uganda mwishoni mwa wiki iliyopita.

Katika mchezo huo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) uliopigwa kwenye Uwanja wa Mandela, mjini Namboole, Kampala, Uganda, timu hizo zilitoka suluhu.

Akizungumza na BINGWA jana, Amunike alisema anatambua uwezo wa wachezaji hao, hivyo akiwapa nafasi katika kikosi chake kuelekea mechi dhidi ya Cape Verde inayotarajiwa kuchezwa Oktoba 10, mwaka huu, wanaweza kuibeba Stars.

“Natambua kikosi changu kipo imara, lakini kama kocha mwenye uzoefu, nimeona pengo la hao wachezaji, kama watapata nafasi, basi nitawapokea, ninaamini watalisaidia Taifa.

“Ninafahamu kuwa ni wachezaji wazuri na wameshaitumikia timu yao ya Taifa kwa muda mrefu,” alisema Amunike.

Wakati huo huo, Amunike amesema baada ya mechi ngumu dhidi ya Uganda, kwa sasa yupo katika mkakati mzito wa kuandaa kikosi chake kwa ajili ya kuisambaratisha Cape Vede kwao.

“Kwa muda huu wachezaji wangu wapo kwenye timu za klabu zao kwa ajili ya mechi mbalimbali za ligi, watakaporudi kambini Septemba 28, nitaendeleza dozi yangu kuhakikisha tunakwenda kufanya vizuri ugenini, ninatumaini hawataniangusha,” alisisitiza Amunike.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*