AMRI SAID ANAVYOFUATA NYAYO ZA PEP GUARDIOLA

NA ZAINAB IDDY

UKIZUNGUMZIA wachezaji waliosakata kabumbu kwa mafanikio na kufanya vizuri kwenye nafasi ya ukocha huwezi kumwacha Pep Guardiola ambaye ameinoa Barcelona, Bayern Munich na sasa Manchester City.

Kocha wa Lipuli, Amri Said, ni mmoja wa makocha ambao wanaonekana kuwa wanaweza kufuata nyayo za Guardiola kutokana na kocha huyo kuifundisha timu hiyo aliyoichezea zamani na kabla ya kujiunga na Simba na sasa anaonekana kuiweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Moja ya mafanikio yake ni kuipandisha timu hiyo ya Iringa na kushika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu, pamoja na kuiwezesha Simba kuwa bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara bila kufungwa mwaka 2019, akiwa kama kocha msaidizi wa Patrick Phiri.

Mwanzoni Amri alionekana kuzipandisha timu nyingi daraja lakini mwenyewe kushindwa kuzifanya zifanye vizuri Ligi Kuu, lakini msimu huu amekuwa tofauti na kuonyesha dalili zote kuwa anaweza kuwa mchezaji mwenye mafanikio kwenye ukocha kama Guardiola.

Historia yake

“Nilianza kucheza mpira kama wanasoka wengine walivyoibuka, nikianzia kucheza  kwenye vitimu vidodo vidogo vya mtaani kama vile Five Stars, Care Boys zote za Kinondoni, Asante Tororo, Tazara, baadaye nikachukuliwa na Lipuli FC ya Iringa hiyo ilikuwa mwaka 1994  na ndipo nilipocheza ligi ya ushindani kipindi hicho ikiwa Ligi Daraja la Kwanza, ikidhaminiwa na Safari Lager kwa msimu mmoja.

“Baadaye nikahamia Majimaji ya Songea mwaka 1995 nilipocheza kwa miaka mitano mfululizo, ambako tukaweza kuchukua ubingwa wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1998 na bao langu ndilo lililotupa ubingwa na hapo ndipo Simba waliponiona na kuvutiwa na mimi, ambapo msimu uliofuata wakanisajili,” anasema.

Anaeleza kuwa akiwa Simba kama mchezaji wa kutumainiwa kikosi cha kwanza, aliweza kuisaidia kuchukua ubingwa  wa Afrika Mashariki na Kati chini ya kocha James Sianga  michuano ikifanyika Zanzibar.

“Mwaka 2003 nikiwa katika kikosi hicho cha Simba tulifanikiwa kuivua ubingwa wa taji la Klabu Bingwa  Afrika timu ya Zamalek ya Misri, kabla ya kuamua kutundika daluga na mwaka 2006.

Kwanini aliacha soka

“Ukocha ni kazi niliyoipenda kuliko kazi nyingine, hivyo baada ya kuona kiwango changu kinapungua uwanjani, majeruhi ya mara kwa mara kutokana na umri kuwa mkubwa nikaona ni bora kugeukia upande mwingine na kusomea ukocha na sasa nimetimiza lengo.

“Wakati naamua kuacha kucheza mpira tayari kuna kozi za awali za ukocha nilishaanza kusomea tangu mwaka 2006 kabla ya kujiendeleza mwaka 2010 na 2014 kusomea beji ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) Daraja C, wakati 2016  nilipata nafasi ya kujiendeleza kwa ngazi ya leseni B ya Caf ambayo ninayo sasa ingawa mipango yangu ni kujiendeleza zaidi.”

Timu alizozipandisha daraja

Katika safari yake ya ukocha Amri ameonekana kuwa na bahati ya kuzipandisha timu kutoka Daraja la Kwanza kwenda Ligi Kuu, ambazo ni  Ndanda FC, Singida United  ambayo aliitoa Ligi ya Daraja la Tatu Mkoa hadi Daraja la Pili.

Nyingine ni Namungo kutoka Daraja la Tatu Mkoa hadi la pili, KMC aliiwezesha kupanda Ligi Kuu lakini walikatiwa rufaa na kupokwa pointi,  hivyo ikasalia Ligi Daraja la Kwanza na nafasi yao kuchukuliwa na African Lyon, pamoja na Mwadui FC aliyofikiskisha Ligi Kuu kipindi hicho akiwa kocha msaidizi akimsaidia Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.

Kumbukumbu zisizofutika akilini kwake

Katika safari yake ya soka akiwa mchezaji yapo mengi ambayo yanafurahisha na kuumiza, lakini jambo ambalo haliwezi kuondoka kwenye akili yake ni kipindi akiwa anataka kusajiliwa na Lipuli FC mwaka 1994, uongozi wa timu ya Tazara aliyokuwa akiicheza uliposhindwa kufuatilia uhamisho wake jambo lililomlazimu kusafiri mwenyewe hadi mkoani Mbeya kwa nauli yake ili aweze kukamilisha jambo hilo zikiwa saa chache kabla ya usajili kufungwa.

“Kwanza sikuwa na fedha kwa kuwa zamani hakukuwa na mshahara katika kazi tunayofanya, lakini nisingeweza kuacha kulifuatilia suala hilo kwa kuwa nilikuwa ninahitaji kujiunga na Lipuli ili niweze kucheza soka la ushindani.

“Hivyo ikanilazimu niombe msaada kwa watu mbalimbali ndipo mtu mmoja aitwaye Razalo Manila, ambaye  kwa sasa ndio Meneja wa Uwanja wa Samora alipoamua kunisaidia kwa kunilipia nauli ya kwenda Mbeya kwenye makao makuu ya Tazara ili kufuatilia uamisho wangu,” anasema Amri.

Anasema:  “Hata baada ya kufanikiwa kuanza kucheza soka la ushindani, bado  kulikuwa na tatizo la kupata nafasi ya kucheza kwani licha ya kujituma, lakini sikuweza kupata nafasi kikosi cha kwanza.”

Ashangazwa na wachezaji wa sasa

Kocha huyo anayeipigania Lipuli hivi sasa iweze kushika nafasi za juu Ligi Kuu Tanzania Bara, anasema anashangazwa na tabia za wachezaji wanaocheza soka hivi sasa hususan wale wa Ligi Kuu ambao wanalipwa fedha nyingi lakini hawana cha maana wanachofanya uwanjani.

“Zamani tulikuwa hatulipwi mshahara, lakini tulicheza kwa kujituma tena kwa mapenzi jambo ambalo vijana wetu wamewashinda kabisa, hii yote ni kutokana na kuangalia fedha zaidi kuliko thamani ya kile kinachowafanya waendeshe maisha yao.

“Mfano kuna wachezaji wanatoka katika timu ndogo kwenda kubwa wakiwa na viwango bora kiasi cha kusajiliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha na kulipwa mshahara mnono, lakini baada ya kucheza mechi mbili tatu wanaanza kupotea na hata kusahaulika kama wapo na hii inatokana na wengi kuendekeza starehe za dunia na kusahau masuala ya soka,”   anasema.

Anatamani kuinoa Simba

“Kama Mungu akijaalia natamani niinoe Simba kama kocha mkuu kwani kwa sasa nainoa Lipuli FC, ambayo ilinitambulisha kwenye soka na sasa akili yangu iko Simba, ambayo nilifanya kazi kwa mafanikio nikiwa mchezaji na hata kocha msaidizi na makocha kadhaa kama Twalibu Hilali, Milovan Cikovich,  Neider dos Santos na Nielsen Elias ambao kila mmoja kwa nafasi yake ameweza kunisaidia kuongeza uzoefu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*