AMEONDOKA SAMATTA, CHILUNDA WENGINE WANAPISHANA KARIAKOO

NA WINFRIDA MTOI

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta anayecheza soka katika timu ya KRC Genk ya Ubelgiji, wiki hii amekuwa gumzo baada ya kuwapo kwa taarifa za kutakiwa na klabu kubwa nne zinazoshiriki Ligi Kuu England.

Habari zilizopo kwa sasa ni kwamba, Samatta ambaye ni nahodha wa timu ya Taifa Stars,  anatakiwa na klabu za Everton, West Ham, Bunrley na Brighton.

Timu hizo zimeeleza kufukuzia saini ya mshambuliaji huyo kuelekea kipindi cha dirisha dogo linalotarajiwa kuanza Januari mwakani.

Katika orodha ya wafungaji wa Ligi ya Ubelgiji ‘First Division A’, Samatta yupo nafasi ya pili akiwa na mabao saba aliyofunga kwa mechi 10 walizocheza, akitoa mchango mkubwa kwa timu yake ya Genk iliyopo nafasi ya kwanza katika msimamo wa ligi hiyo.

Kutokana na hilo, klabu hizo zina haki ya kupigana vikumbo kwa mshambuliaji huyo Mtanzania ukizingatia anacheza katika nchi ambayo iko juu kwenye viwango vya soka duniani.

Ikumbukwe Samatta alijiunga na Genk mwaka 2016 akitokea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambaye  alijiunga nayo mwaka 2011 akitokea Simba.

Ni wazi mafanikio ya mshambuliaji huyo yametokana na juhudi zake mwenyewe licha ya kwamba kuna watu wapo nyuma yake, lakini hawajafanya kazi kubwa  ya kumfikisha hapo alipo.

Samatta amefikia hatua hiyo sasa kwa sababu tangu awali alikuwa amejiwekea malengo tangu alipokuwa anacheza Simba, tena akiwa kijana mdogo, alionekana kuwa na misimamo ya tofauti na wachezaji wengine wanapopata nafasi ya kucheza katika klabu kubwa.

Misimamo na kujiamini ndicho kilichomfikisha Samatta hapo alipo, kwani ni mchezaji ambaye hapendi kuyumbishwa na kushawishika na vitu ambavyo anaona wazi havitamfikisha kule anapotaka, kitu ambacho wamekikosa wachezaji wengi wa Kitanzania.

Wachezaji wengi wanaamini mafanikio ni kucheza Simba na Yanga pekee bila kuangalia mbele, hali inayofanya mwisho wa soka lao kuishia hapa hapa bila kujali thamani ya kile walichokuwa nacho.

Tumeshuhudia wachezaji wengi wakipoteza  vipaji vyao kwa kuyumbishwa na siasa za soka la klabu za Simba na Yanga  ambazo zimekuwa zikiwahitaji kipindi ambacho wanakuwa katika viwango bora, ikitokea kinyume na hapo thamani yao inashuka na kusahaulika kabisa.

Ukiangalia kwa Samatta inaonekana aligundua  kitu hicho mapema na kuchangamkia fursa iliyojitokeza kwake ya kutoka Simba na kwenda  timu ya TP Mazembe ambayo imemfikisha Ulaya na sasa amekuwa lulu na kutakiwa katika ligi yenye mashabiki wengi ya England.

Wakati Samatta akiendelea kung’ara Ulaya, bado kuna wachezaji wanaendelea kuchezea vipaji walivyonavyo wakiridhika na sifa wanazopata kutokana na majukwaa ya mashabiki wa Simba na Yanga.

Naamini Tanzania ina wachezaji wenye vipaji zaidi ya Samata, lakini wameshindwa kujua ni nini wanatakiwa kufanya ili kufikia kule alipo mwenzao.

Kuna baadhi ya wachezaji wanafikia hatua ya kukataa ofa mbalimbali wanazopata za kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kwa sababu tu wanakubalika Simba na Yanga, bila kujua kuwa hali hiyo ina mwisho.

Nawapongeza wachezaji kama Shaaban Chilunda kwa kuchukua hatua mapema ya kuamua kwenda kujaribu changamoto za kucheza soka nchi zenye ushindani na huenda,  baada ya Samatta tukamsikia yeye anahitajika na klabu kubwa Hispania.

Chilunda aliondoka kipindi ambacho timu yake ya Azam FC ilikuwa inahitaji uwepo wake, lakini kutokana na kutambua kipaji chake kinahitaji nini, aliamua kukubali kuondoka.

Tofauti na Chilunda, yupo Simon Msuva, kipindi alichoondoka mchezaji huyo akiwa katika moto na Wanayanga kwa asilimia kubwa, ingekuwa watu wa washiba sifa au kushawishika, asingeondoka kwa sababu angeweza kupewa kiwango chochote cha fedha kutoka kwa Simba waliokuwa wanamfukuzia.

Yapo mambo mengi wanayotakiwa kujifunza wachezaji kama Ibrahim Ajib, Shiza Kichuya na wengine kuwa kipindi chao ni sasa, kutafuta njia ya kutokea kama walivyofanya kina Samatta, Chilunda na Msuva.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*