AMELIZUA

MANCHESTER, England 

KIUNGO wa Manchester United, Paul Pogba, amesababisha mnong’ono mzito kwa baadhi ya mashabiki wa timu hiyo baada ya kuandika kwenye akaunti ya ukurasa wa kijamii wa Instagram ya beki na nahodha wa Juventus, Leonardo Bonucci.

Bonucci alitupia picha ya wachezaji wa Juventus na yeye akiwamo wakisherekea kufuzu hatua ya 16 bora Ligi ya Mabingwa Ulaya jambo ambalo limezua kasheshe mitandaoni.

Kitendo hicho kimewashangaza mashabiki wa Manchester United huku wakijiuliza maswali ya sintofahamu, huenda Pogba yupo mbioni kuondoka, akitajwa mara kadhaa na vyombo vya habari kuhusu uhamisho wake.

Imefahamika Pogba yupo tayari kulazimisha uhamisho wa kurejea Juventus msimu ujao baada ya kukwama kujiunga na Real Madrid kwenye dirisha la usajili majira ya kiangazi, kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka Italia.

Kiungo huyo ambaye yupo nje ya dimba akiuguza jeraha la kifundo cha mguu, amezua gumzo hata kwenye magazeti mbalimbali huko Italia kutokana na alichokiandika kwenye ukurasa huo.

Kwa mujibu wa mtandao wa Tuttosport, Pogba ametamani kurudi Italia kufuatia klabu yake ya sasa (Man United), kutofanya vizuri tangu msimu mpya ulipoanza huku dalili zikionesha mchezaji huyo amechoka na maisha ya jiji la Manchester.

Kwa mujibu wa ripoti, Juventus bado wameendelea kufuatilia hatima ya kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa ambaye ni wazi hana maisha marefu Old Trafford.

Endapo Juventus itamuhitaji Pogba, itawalazimu kutoa kitita cha pauni milioni 110 (sh bil.277) hata hivyo imeripotiwa klabu hiyo haipo tayari kutoa kiasi hicho cha fedha.

Licha ya gharama yake kuwa ndefu, Juventus haijakata tamaa ya kumgo’a Pogba na itapambana kuhakikisha inamnasa msimu ujao.

Pogba ambaye amebakiza mkataba wa miaka miwili Man United, alibeba mataji kadhaa nane akiwa Juventus akiitumikia kwa muda wa miaka sita.

Kiungo huyo alijiunga na Man United mwaka 2016 kwa uhamisho wa pauni milioni 89.3 (sh bil.225) na kuwa miongoni mwa wachezaji ghali zaidi duniani.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*