AMELIKOROGA

LOS ANGELES, Marekani

MASHABIKI wa LA Galaxy ya Marekani, usiku wa kuamkia jana, wamechukizwa na kitendo alichofanya mshambuliaji wao nguli, Zlatan Ibrahimovic, baada ya timu yao kupokea kichapo cha mabao 5-3 kutoka kwa LAFC mchezo wa nusu fainali Kombe la Ligi.

Ibarahimovic alishangaza umati wa watu uliofurika uwanjani baada ya kuonyesha ishara ya kuwadhihaki hususan mashabiki wa LA Galaxy, wakati mechi hiyo ilipomalizika. 

Imedaiwa Ibrahimovic alikerwa na mashabiki wa LA Galaxy waliokuwa wakimnyooshea mikono huku wakimtolea maneno machafu wakati anatoka uwanjani.

Hata hivyo, Ibrahimovic alitoa maelezo kuhusu tukio hilo akidai alichukizwa na walichofanya mashabiki hao.

“Kuna kitu walizungumzia vibaya, sio kama nimefanya kitendo hicho kwa sababu sina heshima, kwanza huu uwanja ni mdogo kwangu, nauona kama sehemu ya mazoezi,” alisema Ibrahimovic.

“Kama nitabaki LA Galaxy itakua jambo zuri kwao, lakini endapo nitaondoka Ligi ya Marekani haitakuwa bora bila ya mimi,” aliongeza.

Kauli hiyo imezua maswali na huenda mechi hiyo ikawa ndiyo ya mwisho kwa nguli huyo ambaye mkataba wake utamalizika Desemba mwaka huu.

Hivi karibu, Ibrahimovic alitajwa mara kadhaa na Rais wa Napoli, Aurelio De Laurentiis, aliyesisitiza anatamani kumuona mshambuliaji huyo raia wa Sweden akijiunga nao itakapofika dirisha dogo la usajili mwakani.

Kigogo huyo alithibitisha kukutana na Ibrahimovic katika hotel ambayo anaishi wakati alipoenda Marekani na kumwalika chakula cha usiku.

Haikuishia hapo, wachambuzi wa soka duniani wameshangazwa kwa kitendo hicho kilichomshushia heshima Ibrahimovic mwenye umri wa miaka 38. 

Mshambuliaji huyo amefahamika kwa tabia zake za kujiamini kupitiliza huku akitoa kauli mbalimbali za kejeli na kujisifia wakati wote.

Ibrahimovich aliwahi kukipiga katika klabu nyingi zikiwamo Manchester United, Barcelona, PSG, Inter Milan na Ajax.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*