googleAds

Ally Ally azinduka, Gustafu si mchezo

NA MICHAEL MAURUS

BEKI mpya wa Yanga, Ally Ally, ameanza kucharuka ndani ya kikosi hicho akionyesha kutokuwa tayari kusotea benchi Jangwani, akifahamu pinzani wake ni Godfrey Paul ‘Boxer’ pekee.

Ally aliyetua Yanga akitokea KMC ya Kinondoni, Dar es Salaam, alianza kwa kusuasua katika mazoezi ya timu yake hiyo mpya yanayoendelea kwenye Uwanja wa Chuo cha Biblia, mjini hapa.

Lakini katika mazoezi ya jana asubuhi na jioni, beki huyo aliyepangwa namba mbili, alifanya vizuri mno, akionyesha uwezo katika kukaba na kupandisha mashambulizi, lakini pia kupiga krosi.

Mchezaji huyo alitua Yanga ili kuongeza nguvu katika nafasi ya beki wa kulia ambayo msimu uliopita ilikuwa na nyota wawili tu, Boxer na Juma Abdul, aliyekuwa akisumbuliwa na wimbi la majeruhi ya mara kwa mara.

Hadi sasa, Abdul bado hajaripoti kambini mjini hapa pamoja na Vincent Andrew ‘Dante’, ikidaiwa wawili hao wamegoma wakitaka wapewe fedha za usajili ndio waungane na wenzao.

Akifahamu kuwa hadi sasa mpinzani wake ni Boxer pekee, Ally ameamua kupiga tizi hasa ili kuepuka kusotea benchi.

Mbali ya Ally, mchezaji mwingine anayekuja kwa kasi mazoezini, ni Simon Gustafu ambaye katika mazoezi ya jana, alicheza vizuri mno, akiwatoa nishai nyota kadhaa, akiwamo Papy Tshishimbi.

Pamoja na kimo chake kifupi, Gustafu mara kwa mara alikuwa akiwazidi ujanja ‘wakongwe’, kwa kuwapora mipira na kuigawa kwa wenzake, akifanya hivyo kwa umahiri wa hali ya       juu, kiasi cha kushangiliwa na mashabiki wachache waliohudhuria mazoezi hayo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*