ALICHOFUATA KEPA CHELSEA NI MATAJI

LONDON, England


KIPA mpya aliyesajiliwa kwa dau la rekodi ya dunia, Kepa Arrizabalaga, amesema anataka kuhakikisha anashinda mataji katika klabu hiyo iliyomnyakua kwa pauni milioni 71.6 kutoka Athletic Bilbao.

Arrizabalaga, alichukuwa nafasi ya kipa Mbelgiji, Thibaut Courtois, ambaye alitangazwa kuwa mchezaji mpya wa Real Madrid juzi Jumatano.

Mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 23, aliichezea Bilbao mechi 57 za ushindani na ilibaki kidogo asajiliwe na Madrid, Januari mwaka huu, lakini dili hilo la pauni milioni 18 lilishindikana.

Akizungumza na mtandao wa klabu, Kepa alikiri kuwa na furaha baada ya kuhamia Chelsea na ana lengo la kushinda mataji.

“Klabu zote duniani zinahitaji makombe na wachezaji wanataka kushinda. Hivyo ninachokihitaji ni kushinda mataji hapa.

“Hicho ndicho ninachotamani kukifanya. Nataka nikumbukwe hapa (Chelsea), nikiondoka nataka watu waseme ‘huyu ni kipa aliyeisaidia klabu kutwaa makombe’.”

Aidha, Arrizabalaga, alimzungumzia kocha mpya wa timu yake hiyo ya Chelsea, Maurizio Sarri, kuwa ndiye chachu iliyomfanya akubali kuondoka Hispania na kuhamia London.

Lakini Sarri naye alinukuliwa mapema wiki hii jinsi anavyomkubali Kepa kwani alikuwa akimfuatilia kwa muda mrefu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*