Ajib atoweka mazoezini Yanga

HUSSEIN OMAR

JANA kikosi cha Yanga kilipiga tizi la kufa mtu katika Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini, huku kikiwakosa nyota wake wanne wa kikosi cha kwanza,  Mrisho Ngassa, Ibrahimu Ajib, Andrew Vicent ‘Dante’, Juma Makapu na Heritier Makambo.

Yanga wanatarajia kuvaana na Mbeya City, Jumatano ijayo katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Lakini katika mazoezi hayo, wachezaji hao watano hawakuwapo wakishindwa kujumuika na wenzao kutokana na kuwa na sababu mbalimbali.

Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, aliliambia BINGWA kuwa wachezaji hao wameshindwa kujumuika katika mazoezi ya pamoja na wenzao kutokana na kusumbuliwa na malaria.

Lakini kwa upande wa Makambo, aliondoka nchini pamoja na Kocha Mwinyi Zahera, ambapo amekwenda Guinea kukamilisha dili la kuichezea Horoya FC na kusaini mkataba wa miaka mitatu.

“Kama hivi ulivyoshuhudia kuna baadhi ya wachezaji hawapo, Makambo ana ruhusa na wengine wana matatizo ya kiafya ndio maana leo wameshindwa kufanya mazoezi,” alisema Hafidh.

Licha ya kutokuwapo kwa nyota hao, lakini Kocha Msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila, alisema amefurahishwa na jinsi wachezaji wake walivyoipokea programu ya leo kwani ana matumaini makubwa ya kufanya vizuri dhidi ya Mbeya City.

“Umeona leo tumejitahidi kufanyia kazi baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza katika michezo iliyopita, lakini pia tumepata nafasi ya kuongeza mbinu mpya kwa ajili ya kumaliza ligi vizuri,’’ alisema Mwandila.

Yanga wanashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na pointi 83 nyuma ya Simba wenye pointi 85, klabu hiyo ya Jangwani imebakiza michezo miwili dhidi ya Mbeya City na Azam wakati mahasimu wao, Wekundu wa Msimbazi wamebakiza michezo minne.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*