Ajib arudi Yanga 

NA ZAITUNI KIBWANA

NAHODHA wa Yanga, Ibrahim Ajib na beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’, wamerejesha tabasamu la mashabiki wa timu hiyo, baada ya kuungana na nyota wengine kwenye safari ya mkoani Morogoro.

Yanga leo itasafiri na wachezaji 20 kuelekea Morogoro kuvaana na Mtibwa Sugar, katika mchezo wa Ligi Kuu utakaochezwa keshokutwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Ajib alikosekana katika kikosi hicho kwenye michezo mitatu ya timu hiyo, akiuguza jeraha la nyonga, huku Ninja akikosekana kwa kutumikia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu.

Akizungumza na BINGWA jana, Mratibu wa timu hiyo, Hafidhi Saleh, alisema wachezaji 20 wataondoka leo, huku Ajib na Ninja wakiwa ni miongoni mwa wachezaji hao.

“Tunaondoka leo kwenda mkoani Morogoro kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Mtibwa Sugar, utakaopigwa Jumatano Uwanja wa Jamhuri,” alisema.

Naye Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera, alisema licha ya kuwakosa wachezaji wake wawili wa kikosi cha kwanza, haimzuii kuibuka na ushindi.

Mkongomani huyo alisema amekuwa akiwapa mbinu mbalimbali wachezaji wake kuelekea mchezo huo wa ligi, ambao anaamini utakuwa mgumu.

“Nitamkosa Kelvin Yondani, ambaye alionyeshwa kadi nyekundu kwenye mchezo wetu dhidi ya Kagera Sugar, pia  Feisal Salum ana kadi tatu za njano, lakini kukosekana kwao hakunipi presha, kwani Ajib amekuwa fiti kiafya pamoja na Ninja,” alisema Zahera.

Wakati Zahera akiyasema hayo, beki wa kulia wa timu hiyo, Paul Godfrey ‘Boxer’ na Andrew Vincent ‘Dante’, wamewataka mashabiki wa timu hiyo kutokuwa na wasiwasi, licha ya kukosekana Kelvin Yondani.

Boxer alisema watakuwa kitu kimoja kuhakikisha kila mchezaji anatimiza wajibu wake ili kusiwepo na dosari ambayo itasababisha faida kwa timu pinzani.

Timu hiyo kwa sasa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi  74, baada ya kushuka dimbani mara 31, ikiwa imeshinda mara 23, sare tano na kupoteza michezo mitatu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*