AJIB AMWITA AMUNIKE U/TAIFA

NA ZAITUNI KIBWANA


STRAIKA wa Yanga, Ibrahim Ajib, amewaalika mashabiki na wadau wa soka akiwamo Kocha Mkuu wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Emmanuel Amunike, kushuhudia mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC utakaofanyika kesho kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Ajib ambaye Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amemtaja kama mchezaji mwenye madini mguuni mwake na kuapa kula naye sahani moja ili kumrejesha katika makali yake, amewapa matumaini makubwa mashabiki na wapenzi wa Yanga kwa kusema kuwa atahakikisha anawapa furaha nyingine wikiendi hii.

Yanga hadi sasa ipo nafasi ya nne baada ya kukusanya pointi 13 ikiwa imecheza michezo mitano, wameshinda minne na sare moja dhidi ya Simba.

Ajib aliyejiunga Yanga akitokea Simba, alieleza kuwa ana historia nzuri ya kuwafunga Mbao na hii haifanyi iwe rahisi kwake kuwafunga tena, lakini amejipanga kufanya hivyo.

“Mechi itakuwa nzuri lakini nitaingia uwanjani kupambana nikiamini naweza kufanya kitu kingine kizuri, japo nafahamu wapinzani nao wana maandalizi,” alieleza.

Wakati Ajib akisema hayo, kocha wa viungo wa Yanga, Noel Mwandila, amesema anaendelea kukinoa kikosi hicho kuhakikisha wanafanya vema kwenye mchezo huo.

“Sisi hatuna wasiwasi kabisa, tunaendelea na maandalizi yetu na timu yetu leo (jana) imeendelea na mazoezi kama kawaida kujiandaa na mchezo huo.

“Tulichokipanga kama benchi la ufundi ni kuhakikisha hatupotezi mchezo hata mmoja, hivyo kamwe hatuwezi kuwadharau wapinzani wowote tunaokutana nao,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*