Ajib ampigia debe Ndemla Yanga

NA ZAINAB IDDY

NAHODHA wa Yanga, Ibrahim Ajib, amesema tetesi za rafiki yake kipenzi, Said Ndemla wa Simba kutakiwa na timu yake zinampa faraja, kwani ataweza kuongeza nguvu kwenye kikosi chao.

Hivi karibuni kumeenea taarifa za viongozi wa Yanga kuwa katika mchakato wa kusaka saini ya kiungo huyo wa Simba anayekipiga kwenye kikosi cha Jangwani.

Ajib ameliambia BINGWA jana kuwa Ndemla kwenda Yanga ni jambo sahihi, ukizingatia hivi sasa hana nafasi katika kikosi cha Simba.

“Ni jambo zuri kwa Ndemla kuja Yanga, kwani itamsaidia rafiki yangu kupata changamoto nyingine, lakini pia atakuwa msaada ndani ya timu yetu,” alisema Ajib.

“Binafsi nimefurahi kusikia hili na naomba Mungu liwe kweli na kwasababu hivi sasa Ndemla hapati nafasi ya kucheza Simba, hivyo ni vizuri kutafuta changamoto sehemu nyingine,” aliongeza Ajib. Kwa sasa Ndemla amekuwa kwenye sintofahamu baada ya dili lake la Sweden alikokwenda kufanya majaribio mara mbili kwenye klabu ya AFC Eskilstuna kuonekana kukwama, huku akikosa nafasi katika kikosi cha Kocha Patrick Aussems. Pia nahodha huyo wa Yanga, aliongeza kuwa kila mchezaji aliyepo katika kikosi hicho ana jukumu la kucheza kwa bidii ili kusaidia timu yao kufanya vizuri. Ajib alisema kwa upande wake, anaamini hata kama mchezaji hajapata ushauri kutoka kwa mwanasaikolojia, lazima atambue majukumu yake yaliyomleta ndani ya timu hiyo. “Ni jambo la faraja kocha kutuletea mtu wa kutuhamasisha, lakini mimi naona kila mmoja anao utimamu wa akili, cha msingi ni kuzingatia ratiba ya mazoezi na maagizo ya kocha na kila jambo litakuwa sawa,” alisema Ajib.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*