AISHI MANULA AMNG’OA MTU MSIMBAZI

NA ABDUL KHALID, TSJ

KAMA ulidhani baada ya kumsajili kipa wa Medeama ya Ghana, Daniel Agyei, zoezi hilo limekamilika, utakuwa umekosea, kwani taarifa mpya zinadai kuwa, wana mpango wa kumtema Vincent Angban na nafasi yake kuchukuliwa na Aishi Manula wa Azam FC.

Kigogo mmoja wa Simba aliliambia BINGWA kuwa, baada ya kushusha vifaa viwili, Angban hatakuwa na nafasi tena, kwani wachezaji wa kigeni watazidi na kufika nane badala ya saba.

“Baada ya kumleta kipa huyo kutoka Medeama na kiungo James Kotei, kuna kila dalili Angban akakatishiwa mkataba wake, kwani wachezaji wa kigeni watakuwa nane badala ya saba.

“Na kwa kuziba pengo lake tupo mbioni kumnasa Aishi Manula wa Azam FC na siku hizi zilizobakia kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa tunaweza kumtangaza kama kipa wetu,” alisema kigogo huyo.

Baada ya Simba kumleta kipa huyo pamoja na Kiungo James Kotei, wekundu hao wa Msimbazi wamefikisha idadi ya wachezaji nane wa kigeni na sasa lazima wamteme mmoja ili wabakie saba.

Mbali na wachezaji hao wawili, wengine wa kigeni waliopo Simba ni Angban, Janvier Bukungu, Method Mwanjali, Jjuuko Murushid, Mussa Ndusha, Frederick Blagnon pamoja na Laudit Mavugo.

Kwa maana hiyo ni kwamba, lazima wapunguze mmoja na kipa Angban ndiye ambaye jina lake limewekwa kwenye mstari mwekundu na nafasi yake huenda ikachukuliwa na Manula.

Baada ya taarifa hizo kuvuja, BINGWA lilikwenda mbali na kumtafuta Manula, ambaye alisema hana taarifa zozote kuhusu kutakiwa na Simba na kama wana mpango huo wazungumze na timu yake.

“Kwasasa mimi ni mchezaji wa Azam na kama Simba wanataka huduma yangu, basi wakae mezani na timu yangu waelewane,” alisema Manula.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*