AFADHALI WAZUNGU WAMEANZA KUELEWA KANUNI BORA YA USAJILI

WIKIENDI iliyopita tulibarikiwa vilivyo na soka. Kubwa zaidi ni mtanange wa Ngao ya Jamii kati ya Manchester City na Chelsea uliochezwa jana.

Wachambuzi wa soka wameshamaliza kuzungumza mengi kuhusu mechi hiyo pamoja na nyingine za kirafiki.

Kilichobaki ni kusubiri ligi kubwa duniani zianze kutimua vumbi wikiendi hii hadi mwakani.

Tangu Kombe la Dunia lilivyomalizika, usajili ulizidi kushika hatamu na ndio maana nimeona niendelee kuzungumza zaidi kuhusu hilo wakati timu zikijiandaa kuanza ligi.

Timu nyingi maarufu duniani zimeshajipatia wachezaji wao na uhamisho mkubwa wa siku chache zilizopita ni wa Arturo Vidal kutoka Bayern Munich kwenda Barcelona.

Vidal ni mmoja wa wachezaji zaidi ya 3000 wa kimataifa ambao wamehama kutoka timu moja kwenda nyingine baada ya dirisha kufunguliwa Juni hadi Julai mwaka huu.

Wachezaji hao wamegharimu zaidi ya Dola Trilioni 2.7 ndani ya mwezi huu tu. Kwa mujibu wa Ripoti ya FIFA TMS: JULAI 2018.

Nimeisoma vyema ripoti hiyo, imeeleza kwa kuzingatia namba kwamba hakuna mabadiliko makubwa sana kutoka ripoti ya Julai 2017.

Lakini kuna sehemu kadhaa katika ripoti hiyo zilinipa fursa ya kuvitafakari na angalau, kusema neno.

England kwa mara nyingine tena imekuwa nchi iliyotoa na kuingiza wachezaji kwa wastani mkubwa sana. Imefanikwa kuingia katika tano bora ya mataifa yaliyofanya biashara kubwa ya wachezaji kwa mwezi.

Ni kituo kikubwa cha biashara ya soka. Wana nguvu kubwa sana ya ushawishi kwa wachezaji, nashawishika kukubaliana na hilo kwa mujibu wa namba za usajili zilivyosema.

Ripoti ya Julai mwaka jana ilionyesha kuwa waliingiza jumla ya wachezaji 248 lakini mwaka huu wameingiza 214. Pungufu ya watu 34 tu ambao si wengi sana lakini itawatia moyo hata wao wenyewe.

Kwanini watajisikia faraja? Kwa heshima yenu naomba nitumie mfano wa klabu ya West Ham.

West Ham ilianza kuajiri kocha mpya, Manuel Pellegrini, halafu likafuatia zoezi la kusajili wachezaji.

Uamuzi wa kwanza ni mzuri sana, Pellegrini ni mzoefu wa Ligi Kuu England, atawasaidia ‘The Hammers’ kurejea kwenye mstari mnyoofu.

Uamuzi wa pili wa kuongeza wachezaji kadhaa ambao wana uzoefu wa kucheza soka la ushindani katika ligi kuu tano kali za Ulaya, ni bora.

Hawakuchukua wachezaji wengi kwa sababu kikosi chao hakijapukutika sana kutoka msimu uliopita ambao walimaliza ligi nafasi ya 13.

Si ajabu kwao. Katika misimu sita iliyopita wana wastani wa kumaliza katika nafasi ya 12. Hivyo ilitakiwa akili ya ziada kuhakikisha usajili unaofanyika ni wenye mantiki.

Wameachana na wachezaji wanne. Wawili ni ‘wahenga’.

Mmoja alicheza kikosi cha kwanza msimu uliopita na kinda mmoja.

Wamesajili wachezaji saba. Asilimia kubwa ya wachezaji hao moja kwa moja wataingia kikosi cha kwanza.

Wawili kati yao wamewapata bure, wawili wameigharimu klabu pauni milioni 29. Wengine ada za uhamisho wao hazikuwekwa wazi.

Mmoja wa wachezaji hao ni Felipe Anderson. Mbrazil aliyehusishwa sana na Manchester United miaka kadhaa iliyopita.

West Ham wamegharamikia pauni milioni 35 kuipata saini ya Anderson. Na watamlipa mshahara wa pauni 85,000 kwa wiki. Lazio walikuwa wanamlipa Anderson mshahara wa pauni 55,000 kwa wiki.

Kwanini sasa England watafarijika na ripoti ya TMS. Angalau wazungu wanaoziongoza klabu zao wamejifunza kwamba si tu kusajili wachezaji wa kutosha watakaosaidia vikosi vyao, bali pia kulipa mishahara mizuri.

Kuna kila dalili West Ham ikafanya vizuri zaidi msimu ujao kwa walichokifanya kwa Anderson na wenzake waliosajiliwa katika dirisha hili la majira ya kiangazi.

Japokuwa, suala la wachezaji kulipwa mishahara mizuri halijaanza mwaka huu tu. Mfano, mwaka 2014, Paul Pogba akiwa Juventus alikuwa analipwa pauni 23,000 tu kwa wiki, alivyorudi England, United ‘wakamchapa usoni’ na pauni 290,000 kwa wiki!

Kevin De Bruyne sasa analipwa pauni 350,000 kwa wiki, awali alikuwa analipwa pauni 115,000 kwa wiki.

Hivyo suala kuu hapa si tu kulipa mishahara mizuri kwa kujaribu, bali kwa uhakika ili kuwafanya wachezaji wawe na morali ya kusaka mataji bila kunung’unika.

Kulazimisha usajili wa gharama kubwa ulete mafanikio ni janga kubwa sana na limezikumba klabu nyingi za soka hasa za England. Zinanunua wachezaji wengi kwa gharama kubwa lakini mafanikio yanayopatikana ni madogo.

Kama ripoti ya TMS Julai mwaka jana ilivyoeleza idadi kubwa ya wachezaji walioingia England lakini mafanikio makubwa zaidi yaligawanyika kwa klabu chache kati ya zile kubwa ambazo zilitikisa soko la usajili.

Manchester City walishinda ligi kuu na Carabao. Chelsea walichukua FA. Liverpool walifika fainali ya Ligi ya Mabingwa wakalikosa kombe. Man United walifika fainali FA. Arsenal walifika nusu fainali Ligi ya Europa.

Angalau Man City na Man United zimejitahidi sana kulipa mishahara minono hivyo ni jukumu lao kuwa na mwendelezo mzuri, na faida itawajia muda mfupi ujao.

Historia ipo wazi sana. Usajili wa gharama kubwa hauna nguvu ya kuifanya timu iweze kumaliza kwenye nafasi ya juu na kutwaa mataji. Hutokea ndio lakini ni nadra kuwa na mwendelezo. Mishahara mizuri kwa wachezaji wanaosajiliwa ndio siri ya mafanikio.

Real Madrid haikufanya matumizi makubwa sana ya usajili msimu uliopita, namba zao katika fedha walizotumia zimepanda kati ya Juni na Julai mwaka huu tu lakini waliweza kushinda mataji matatu makubwa Ulaya (labda mawili).

Kubwa zaidi ni kuhakikisha wanalipa kikosi cha kwanza fedha nzuri ya mshahara kwa wiki, hasa wale wazalishaji wakubwa wa matokeo, nawazungumzia washambuliaji. Gareth Bale na Cristiano Ronaldo ndio walikuwa wanachukua mshahara mnono msimu uliopita.

Na bado Hispania hawajawa tishio kwa England katika matumizi makubwa ya fedha kwenye usajili. Ligi yao imetupwa mbali sana ukiangalia ripoti ya TMS Julai mwaka jana na mwaka huu.

Mwaka huu thamani ya usajili uliofanyika England ni dola milioni 730, mwaka jana ilikuwa milioni 733.

Labda baada ya dirisha la usajili wa mwaka huu mambo yatabadilika na tutaona timu za England zikifanya vizuri zaidi baada ya kufanya biashara yenye tija.

Na matumaini yangu hayo yanachagizwa zaidi na ripoti ya TMS ambayo ilieleza zaidi kwamba idadi ya wachezaji waliotoka England kwenda ligi nyinginezo kati ya Juni na Julai mwaka huu ni 195, tofauti na 237 waliohama mwaka jana.

Siri nyingine ya timu kuendelea kubaki katika kiwango cha juu ni kubakiza wachezaji wake muhimu. Mfano mzuri Tottenham Hotspurs. Mwaka huu timu nyingi za ligi hiyo zimefanikiwa kubakiza wachezaji wao muhimu.

Mohamed Salah alihusishwa sana kwenda Real Madrid, amebaki Liverpool. Eden Hazard, Thibaut Courtois, naziona dalili zao za kuendelea kukipiga Chelsea.

Unakumbuka tetesi za Harry Kane kuikacha Spurs na kwenda Real Madrid, zimeshazimika tayari. Dele Alli naye, Christian Eriksen kwenda Barcelona, Hector Bellerin wa Arsenal, alitikisa sana kutakiwa na Barca.

Wote hao wanaendelea na timu zao kama kawaida, jinsi gani wazungu walivyoshinda majaribu ya soko la usajili kwa kutofanya biashara kichaa kama miaka iliyopita na kutumia kanuni bora ya kulipa mishahara mizuri.

Iwapo tu soko la usajili linatawaliwa na biashara ya kizembe-zembe, lazima klabu nyingine chache zipate fursa ya kufanya biashara yenye akili.

Klabu nyingi zinavyopoteza fedha kwa usajili wa gharama kubwa, basi kuna klabu zitatumia akili kusajili na zitafanya vizuri kwenye mashindano.

Kidogo wazungu wamejifunza, sio sana. Huko mbele wataelewa zaidi kadiri timu zao zitakavyokuwa zinatumia fedha kijinga kwenye usajili na hazipati mafanikio ya kueleweka.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*