Kila la heri Simba

WEKUNDU wa Msimbazi, Simba, leo watashuka dimbani kupambana na AS Vita ya Kongo katika mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba, yenye pointi tano, ilikuwa kundi D pamoja na timu ya JS Saoura ya Algeria, inayoongoza kundi ikiwa na pointi nane, Al Ahly ya Misri pointi 7 sawa na AS Vita.

Wawakilishi hao pekee wa Afrika Mashariki na Kati katika michuano hiyo mikubwa Afrika, walifika hatua ya makundi baada ya kuziondosha timu za Mbambane Swallows na Nkana katika hatua ya awali na kufanikiwa kuingia makundi.

Katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya JS Saoura Dar es Salaam, Simba iliitandika timu hiyo bao 3-0, lakini ilikula kichapo katika michezo yake miwili iliyofuata dhidi ya Vita huko Kongo na Ahly nchini Misri kwa idadi sawa ya mabao 5-0 katika mechi hizo.

Simba ilikuja kuzinduka Uwanja wa Taifa wakati ikimfunga mgeni wake, Ahly bao 1-0, lakini ikaenda kupoteza Algeria kwa kukubali kipigo cha bao 2-0 dhidi ya Saoura.

Matumaini ya Simba kufuzu katika hatua ya robo fainali yamebakia kwa Vita, ambao watamenyana nao Uwanja wa Taifa saa 1:00 usiku wa leo.

Viongozi wa Simba wakishirikiana na benchi la ufundi, chini ya Kocha Patrick Aussems, wamejipanga vilivyo kuhakikisha Simba inakwenda katika hatua nyingine kubwa ya robo fainali.

Wachezaji wa Simba pia wamejinasibu kuwa hawatawaangusha mashabiki wao kwa kukubali kupigwa katika uwanja wao.

Tangu kuanza kwa michuano hii, Simba imeweka historia ya kutofungwa katika uwanja wake wa nyumbani, hali inayotishia amani kwa vigogo wa soka Afrika.

Katika kujiandaa na mechi hii, Simba wamekuja na kauli mbiu mpya ya ‘Do or Die’, ambayo imewapa hamasa kubwa mashabiki wa timu hiyo ambao bado wana msemo wao ulioshika kasi wa ‘Yes We Can’.

Sisi BINGWA tunawatakia kila la heri Simba katika harakati zao za kuwatoa kimasomaso Watanzania, huku tukiamini waliyoyapanga katika mechi hiyo yanawezekana.

Itakuwa faraja kubwa kwa Watanzania kuona timu zao zimebadilika na kuanza kufanya vizuri kimataifa.

Ni ombi letu kwa Watanzania, waende uwanjani wakiwa na moyo wa kizalendo, kwani mafanikio ya Simba ni ya Watanzania wote, kwakuwa wakiendelea kufanya vizuri timu nyingine za Tanzania zitapata faida.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Simba.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*