PATACHIMBIKA

LONDON, England


 

MICHUANO ya Ligi Kuu England inaendelea leo katika viwanja saba tofauti, ambapo miamba 14 inayoshiriki michuano hiyo itakuwa ikisaka pointi tatu muhimu kwa ajili ya kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa na kushiriki katika mashindano makubwa Ulaya.

Mechi hizo ni pamoja na itakayoikutanisha Bournemouth dhidi ya Man United, Cardiff dhidi ya Leicester, Everton itakayoivaa Brighton, Newcastle watakaokuwa wenyeji wa Watford, West Ham ambao watakuwa nyumbani wakioneshana ubavu na Burnley,  Arsenal dhidi ya Liverpool na Wolves ambao watatoana jasho na Tottenham.

Hata hivyo, pamoja na kila mechi hizo kuwa na msisimko wa aina yake, lakini ya Arsenal dhidi ya Liverpool ndiyo itavuta hisia za mashabiki wengi kufuatia kila timu inao wengi.

Mtanange huo ambao utapigwa katika Uwanja wa Emirates, kila timu itaingia dimbani ikiwa na dhamira tofauti kwani mpaka sasa timu hizo hazipishani bali  kwa pointi kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Arsenal mpaka sasa imeshajikusanyia pointi 22 ilizovuna kwenye mechi 10 na inashika nafasi ya nne, wakati Liver wao wana 26 walizokusanya kwenye mechi kama hizo na wapo nafasi ya pili, hivyo Gunners watakuwa na kiu ya kuhakikisha wanashinda mtanange huo ili wahakikishe wanabakiza pengo la pointi moja.

 

Mbali na hilo, mechi hiyo pia inatarajiwa kuwa na utamu wa aina yake kufuatia kuwa baada ya kupoteza mechi zake za kwanza dhidi ya Manchester City na Chelsea, vijana hao wa kocha Unai Emery, walizinduka na kuanza kutembeza vipigo kwa kucheza mechi 13 bila kufungwa.

Hata hivyo, pamoja na Gunners kuonekana kuwa imara kwa sasa, lakini inaweza kukutana na kigingi kwani inakutana na Reds ambayo nayo haijapoteza mchezo hata mmoja kwenye ligi kama wao ambao wameshachapwa mara mbili.

Kati ya michezo mitatu iliyopita, miamba hiyo ilitoka sare miwili jambo ambalo linawafanya mashabiki wengi kushindwa kutabiri ni timu ipi itaondoka uwanjani kifua mbele.

Hata hivyo, Arsenal wanakabiliwa na tatizo la kuwa na majeruhi wengi ikilinganishwa na wapinzani wao, baada ya nyota wake tegemeo kama vile Hector Bellerin, Nacho Monreal na Sead Kolasinac itawalazimu kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu wakikabiliwa na majeraha na huku wengine, Mohamed Elneny, Konstantinos Mavropanos na  Laurent Koscielny hali zao zikiwa bado ni tete.

Kwa upande wao Liver, watawakosa nyota wao wawili, Jordan Henderson na Naby Keita ambao nao bado wanaendelea kuuguza majeraha yao ya misuli ya nyama za paja.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*