MMACHINGA ALIINUSURU YANGA KUFUNGWA NA COFFEE 1998

NA HENRY PAUL


UNAPOZUNGUMZIA wachezaji wa zamani waliopata mafanikio katika soka, kamwe huwezi kuacha kulitaja jina la mshambuliaji wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’.

Mmachinga aliyejiunga na Yanga katika  miaka ya 1990 akitokea Klabu ya Bandari ya Mtwara, ambaye alikuwa mshambuliaji mahiri wa kutegemewa kwa kupachika mabao muhimu katika timu hiyo na kupata mafanikio.

Miongoni mwa mafanikio nyota huyo aliyofanya ni kuiwezesha timu hiyo kupata sare ya mabao 2-2 dhidi ya Coffee FC ya Ethiopia, mchezo uliochezwa Aprili 26, 1998  kwenye Uwanja wa Taifa, mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Mechi hiyo ambayo ilikuwa ni kali na ya kusisimua muda wote wa dakika 90, ilikuwa ni ya kwanza raundi ya pili, michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Matayarisho ya mchezo huo yalikuwa ni mazuri, kwani Yanga walifanya mazoezi ya kutosha takribani mwezi mmoja hivi chini ya kocha wao mkuu, Tito Mwaruvanda aliyekuwa akisaidiana na Fred Felix ‘Majeshi’.

Mechi hiyo ilianza kwa kasi huku timu ya Coffee ikilishambulia lango la Yanga kwa mashambulizi makali kuanzia dakika ya kwanza ya mchezo na mashabiki wa timu hiyo ambao walikuwa wamejazana uwanjani siku hiyo, wakiishangilia kwa nguvu timu yao.

Baada ya Coffee kuishambulia Yanga kwa kipindi kirefu kidogo, dakika ya 15 walifanya shambulio moja la nguvu na kufanikiwa kupata bao la kuongoza.

Baada ya timu hiyo ya Ethiopia kupata bao hilo, hawakuishia hapo, kwani waliendelea kulisakama lango la Yanga huku mabeki wakionekana kuwa na kazi moja ya kudhibiti mashambulizi hayo.

Mashambulizi hayo yalizaa matunda kwani dakika ya 30, Coffee walifanya shambulizi jingine la nguvu langoni kwa Yanga na kufanikiwa kupata bao la pili ambalo lilipatikana baada ya washambuliaji wa timu hiyo kugongeana vizuri.

Baada ya bao hilo, Yanga walizinduka  dakika ya 40 na kuanza kulishambulia lango la wapinzani wao.

Katika mashambulizi hayo, winga wa kulia, Akida Makunda, alichukua mpira pembeni na kupiga krosi iliyomkuta Sekilojo Chambua aliyefunga bao la kwanza kwa kichwa.

Mpaka dakika 45 zinamalizika timu zilikwenda mapumziko Coffee wakiwa mbele kwa mabao 2-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa Coffee kupunguza kasi tofauti na walivyoanza, hivyo kuwapa mwanya Yanga kufanya mashambulizi ya mfululizo.

Mashambulizi ya Yanga yaliwanufaisha, kwani dakika ya 65 walifanya shambulizi zuri langoni kwa wapinzani wao na kufanikiwa kusawazisha.

Bao hilo lilifungwa na Mmachinga  aliyefunga kwa kiki kali lililokwenda kutinga wavuni, huku kipa wa Coffee akijitahidi kudaka bila ya mafanikio.

Baada ya Yanga kusawazisha bao hilo, mchezo ulibadilika kwa timu kushambuliana kwa zamu.

Yanga: Joseph Katuba (marehemu), Mzee Abdallah, Kenneth Mkapa, Paul John, Abdallah Msheli, Banza Tshikala, Akida Makunda, Iddi Moshi ‘Mnyamwezi’, Sekilojo Chambua, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ na Edibily Lunyamila.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*