MSUVA ATHIBITISHA KUPATA OFA KIBAO ULAYA 

NA WINFRIDA MTOI


WINGA wa zamani wa Yanga anayekipiga katika timu ya Difaa El Jadida ya nchini Morocco, Simon Msuva, ameweka wazi kuwa safari yake ya kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya imekaribia kutokana na ofa anazozidi kupata.

Kwa muda mrefu Msuva alikuwa akihusishwa na timu mbalimbali za Ulaya ikiwamo za nchini Hispania kutokana na kiwango anachokionyesha katika timu yake Difaa El Jadida.

Akielezea mipango yake hiyo kwa njia ya mtandao, Msuva aliliambia BINGWA kuwa, Msuva kutokana na ofa anazopata haitachukua muda mrefu kuondoka ndiyo sababu amekuwa akicheza kwa juhudi na kujituma zaidi.

“Nafanya kazi kwa kujituma kwa kuwa ndoto zangu ni kufika Ulaya ninapotaka, Samatta (Mbwana) tayari amefika mbali lakini nitamfuata, ni suala la muda tu naamini Mungu atanisaidia nitakwenda kupambana.

“Ofa zimejitokeza ila kikubwa ni kukaa pamoja mezani na kuzungumza kwa sababu bado nina mkataba na timu yangu,” alisema Msuva.

Hata hivyo, Msuva alisema kinachompa morali zaidi ni baada ya kuona hivi karibuni mtu mmoja kutoka Ulaya ametengeneza picha yake akiwa amemuunganisha na Sagio Mane wa Liverpool na kumwambia inakuwaje huyu yupo Ulaya na wewe haupo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*