ZAHERA ACHIMBA MKWARA YANGA

NA TIMA SIKILO


KOCHA wa Yanga, Mwinyi Zahera, amewachimba mkwara mzito nyota wake akisema kwamba, kitendo cha mchezaji kutofanya kazi yake ipasavyo akiwa uwanjani na kumbebesha majukumu kipa, kitawafanya wengi wa kikosi cha kwanza kusugua benchi.

Kauli hiyo ameitoa kutokana na baadhi ya wachezaji kushindwa kufanya kile wanachotakiwa, badala yake kumbebesha mzigo kipa ambaye naye ana kazi kubwa langoni.

Akizungumza na BINGWA, Zahera alisema hana hofu hata kidogo kuacha kumtumia mchezaji nyota ambaye hatekelezi majukumu yake anapokuwa uwanjani, kwani jukumu lake la kwanza ni kuhakikisha kila mchezaji anafanya kinachotakiwa.

Alisema kikosi chake kina wachezaji wengi ambao watu wanapenda kuwaona wakifanya vizuri kila siku uwanjani, lakini jambo hilo ni tofauti kwake kwani licha ya kufanya vizuri anahitaji nidhamu na kujituma mazoezini ili aweze kumtumia mchezaji.

Aidha, aliongeza kwamba wachezaji wengi ni wazito mazoezini kwani hawatekelezi kile anachowatuma na hata wanapokuwa uwanjani wanafanya hivyo hivyo, sasa kwa hali hiyo benchi litawahusu hadi watakapokaa sawa.

“Mimi siangalii jina naangalia uwezo na uwajibikaji wa mchezaji, kama anafanya vibaya siwezi kumtumia na kumchezesha mtu ambaye kazi yake inafanywa na mwingine anapokuwa uwanjani,” alisema Zahera.

Hata hivyo, Zahera alisema pamoja na hali ngumu ya kiuchumi kuikumba timu hiyo, anajitahidi kuhakikisha mwaka huu wanachukua ubingwa.

“Hali ya kifedha si nzuri lakini hilo haliwezi kutuvunja moyo, tutacheza mwanzo mwisho kupata matokeo na mwisho wa siku kuwa mabingwa, ’’ alisema Zahera.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*