WADAU, MASHABIKI WANAVYOWAPA MSONGO WA MAWAZO WASANII

NA CHRISTOPHER MSEKENA

MIONGONI mwa mijadala mikubwa katika tasnia ya burudani nchini, ni wasanii wapya wa Bongo Fleva kupewa nafasi kubwa zaidi ya kusikika kuliko wale walioanza muziki muda mrefu.

Ni ukweli usio na shaka kuwa muziki wa sasa umetawaliwa na nyimbo nyingi ambazo zimeimbwa na wasanii waliotoka kimuziki miaka ya hivi karibuni huku wale waliotoa miaka 15 kurudi nyuma ni wachache sana wanaosikika.

Tazama chati za muziki mbalimbali nchini utagundua hilo jambo ambalo halipendezi na linatengeneza chuki kutokana na hali halisi ya maisha ya sanaa ambayo kwa sasa imekuwa ni ajira, hivyo kutowapa nafasi wasanii wa muda mrefu ni sawa na kuwanyima ujira.

Wasanii wa muda mrefu walishiriki kutengeneza njia ambayo sasa hivi wasanii wapya wanaitumia kutengeneza muziki ambao unafanyika biashara hivyo kuwaingizia kipato wanachoendeshea maisha yao.

Heshima ya wasanii hao wa kitambo imekuwa haionekani sana kama ambavyo ilitakiwa iwemo hali ambayo inawaweka mbali na biashara ya muziki inayoendelea sasa kwenye sekta ya muziki.

Hatua hiyo inafanya wasanii wa muda mrefu ambao walikuwa wanategemea muziki kujiingizia kipato bila kuwa na shughuli nyingine kujiingiza katika mitindo ya maisha inayokuja kugharimu maisha yao.

Mara nyingi tumesikia wasanii wa Bongo Fleva wakiingia katika utumiaji wa dawa za kulevya kutokana na msongo wa mawazo unaotokana na kutopewa nafasi tena katika kiwanda cha muziki.

Huku wasanii hawa wa muda mrefu wakishuhudia wadogo zao wakitengeneza fedha nyingi kutokana na muziki wanaoufanya wakati kipindi kile wanavuma hakukuwa na mazingira ya biashara yaliyopo sasa.

Mbaya zaidi wanaitwa majina yenye nia ya kuwapoteza kabisa. Jina kama mkongwe limekuwa likiwaudhi wasanii wa muda mrefu kutokana na kulenga zaidi kuwaonyesha kuwa ni toleo la zamani hivyo si chochote kitu katika zama hizi.

Mashabiki wamekuwa wakipokea majina hayo na kuyafanyia kazi kwa kuweka mipaka baina ya wasanii wapya na wale wa muda mrefu, hivyo hata msanii wa zamani akitoa kazi haipati mapokezi stahiki hata kama ni kazi nzuri.

Hali hiyo imekwenda sambamba na tabia ambayo ipo duniani kote ya kutowakubali wasanii wakiwa hai ila inapotokea wamekufa ndiyo wadau na mashabiki wanaunga mkono kwa nguvu zote kazi zao.

Mtindo huo huwapelekea wasanii kuingia katika msongo wa mawazo kiasi cha kujiingiza kwenye matukio ambayo matokeo yake ni kupoteza maisha au kuishia sehemu mbaya.

Miongoni mwa watu ambao enzi za uhai wake walikutana na changamoto kama hizo ni prodyuza Joshua Magawa ‘Pancho Latino’ ambaye aliwahi kusema wadau na wasanii aliowasaidia kimuziki hawampi tena ushirikiano kama ilivyokuwa zamani kitu ambacho kilifanya asione thamani yake na kuingia katika msongo wa mawazo.

Bado tuna nafasi ya kurekebisha hili ili sekta ya sanaa itoe ajira kwa wasanii wote wale wa muda mrefu na hawa wapya kwa sababu msanii anategemea kipaji chake ili aendeshe maisha na anaweza kufanya hivyo endapo atapewa ushirikiano kutoka kwa wadau na wewe shabiki.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*