googleAds

Diamond ampeleka Hawa kutibiwa India

Bethsheba Wambura, Dar es Salaam

Hatimaye msanii Hawa Ramadhani, aliyekuwa mpenzi wa staa wa Bongo fleva Naseeb Abdul maarufu Diamond, amefanikiwa kwenda nchini India kwa matibabu ya ini.
Hawa ambaye matibabu yake  yamegharamiwa na Diamond, ameondoka leo Jumamosi Oktoba 13, kwa ndege ya Emirates.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Meneja wa Diamond, Hamis Tale maarufu Baba Tale, ambaye anasafiri naye kwenda India akiambatana na mama yake Hawa, amesema gharama za matibabu kabla ya kubadilisha ini ni Dola za Marekani 20,000.
“Lakini tukitaka abadilishiwe gharama zake ni Dola 42,000, tutajaribu tutakapoweza na tukishindwa tutaomba msaada kwa Watanzania watusaidie peke yetu hatutaweza.
“Tulikuwa tunajua kama anaumwa ila tukawa tunashindwa kujua tunaanzaje kumsaidia, tulipoona katika mitandao tukajua hali ni mbaya, Diamond alinitafuta akaniambia bosi nisaidie kupata njia nzuri ili niweze kumsaidia Hawa, basi tukafanya utaratibu na siku imefika leo tunaenda India,” amesema Babu Tale.
Aidha, Babu Tale amesema, wakati Hawa anatumia madawa ya kulevya alimfuata kutaka kumsaidia lakini alikataa ila kuna dada ana kituo cha kusaidia wenye uraibu wa dawa za kulevya (sober house), ndiyo alimsaidia kumchukua.
“Hatujui matibabu yatachukua muda gani Mungu na madaktari ndiyo wanajua, cha muhimu ni Watanzania kumuombea Hawa arudi salama, ”.
Taarifa za kuumwa kwa Hawa, zilitangazwa kwa mara ya kwanza na chaneli ya Youtube ya Mtanzania Digital kuwa msanii huyo ambaye anasumbuliwa na ini na tumbo lake kujaa maji anahitaji msaada wa matibabu.
Hawa na Diamond ambao waliwahi kuimba pamoja wimbo wa Nitarejea, wanadaiwa kuwahi kuwa wapenzi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*