TSHISHIMBI AREJEA KIVINGINE

NA HUSSEIN OMAR

SI unakumbuka ule moto alioanza nao kiungo fundi wa Yanga, Papy Tshishimbi, alipojiunga na timu hiyo? Sasa jamaa amerudi kivingine na makali zaidi ya yale ya awali.

Tshishimbi alilazimika kukosa baadhi ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, kutokana na majeraha aliyokuwa nayo lakini sasa amerejea kijeshi kuokoa jahazi.

Kiungo huyo ambaye baada ya kupata majeraha alilazimika kukaa nje ya uwanja kwa ajili ya matibabu, alizua hofu miongoni mwa mashabiki kutokana na kiwango chake lakini kuanza kwake kujifua kumeshusha presha.

Katika baadhi ya michezo ambayo Tshishimbi amecheza msimu huu, alionyesha kiwango duni kiasi cha kumfanya kocha wake, Mwinyi Zahera, kumshushia lawama kila mara.

Kwa sasa Tshishimbi ameanza kujifua huku akionekana kuwa na usongo wa hali ya juu hali inayotoa ujumbe kwa mashabiki wao kwamba wakae mkao wa kula.

Akizungumza na BINGWA jana, mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kiungo na beki Juma Abdul wamerejea na kuanza mazoezi ya pamoja wenzao.

“Mambo ni mazuri, wachezaji waliokuwa majeruhi Tshishimbi na Abdul wapo mazoezini sasa kazi kwao kuwashawishi makocha wawapange katika michezo ijayo,” alisema Hafidh.

Alisema kikosi cha timu hiyo kiliendelea na mazoezi yake jana katika Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini, Dar es Salaam ikiwa ni maandalizi kwa ajili ya mechi zao za Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Timu ipo vizuri na jana asubuhi tumeendelea na ratiba ya mazoezi, tunaomba mashabiki wetu waendelee kutusapoti tupo kwa ajili ya kuwapa burudani,” alisema Saleh.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*