googleAds

ETO’O AMFUATA AMUNIKE DAR

NA MWAMVITA MTANDA

Wakati Kocha Mkuu wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Emmanuel Amunike, akiwaonya wachezaji wake kuelekea mchezo dhidi ya Cape Verde, kuna habari kuwa nyota wa zamani wa Cameroon, Samuel Eto’o, muda wowote kuanzia sasa anatua nchini.

Habari kutoka kwa mmoja wa marafiki wa Eto’o, aliposti jana katika mtandao wake wa Instagram kuwa nyota huyo wa zamani wa Barcelona, anatarajia kutua Tanzania wiki hii.

“Nimeongea na Eto’o ameniambia wiki ijayo (hii), atakuwa Afrika Mashariki katika Jiji la Dar es Salaam,” aliposti rafiki huyo wa Eto’o aliyetambulika kwa jina la Joseph N.

Hata hivyo, haijafahamika Eto’o anakuja Tanzania kwa shughuli gani japo BINGWA linaamini anaweza kukutana na Amunuike iwapo kocha huyo wa Stars atakuwapo hapa nchini kabla mkali huyo wa Cameroon hajaondoka.

Amunike na Eto’o ni miongoni mwa wachezaji wa Afrika waliowahi kutamba Ulaya, wote hao wakiwa wameichezea Barcelona ya Hispania katika vipindi tofauti.

Wakati huo huo, Amunike amesema ili kikosi chake cha Stars kifanikiwe kupata ushindi dhidi ya Cape Verde katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon2019) Oktoba 12, mwaka huu, wachezaji wake lazima wazingatie mambo ya msingi anayowafundisha, ikiwamo nidhamu ya mchezo.

Akizungumza na BINGWA jana, Amunike alisema pia vijana wake hao wanatakiwa kuwa na kasi ya mchezo pamoja na kujiamini.

“Timu ambayo tunakwenda kukutana nayo ni mgumu sana, asilimia kubwa ya wachezaji wao ni wa kimataifa, hivyo watakuwa na kasi ya kutosha,” alisema Amunike.

Amunike alisema iwapo watafanikiwa kushinda mechi hiyo ya ugenini, watakuwa na uwezekano mkubwa wa kufanya vizuri katika michezo mingine inayofuata ya michuano hiyo.

Stars iliyopo Kundi L la michuano hiyo, imejikusanyia pointi mbili baada ya kutoka sare na Uganda (ugenini) pamoja na Lesotho (nyumbani).

Kikosi cha Stars kinatarajiwa kuondoka hapa nchini kesho kuifuata Cape Verde tayari kwa pambano hilo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*