googleAds

DIRISHA DOGO CHUNGU KWA KLABU

NA WINFRIDA MTOI

Kamati  ya Leseni za Klabu Tanzania imezitangazia kiama Klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara, kuwa ifikapo dirisha dogo klabu yoyote isiyokuwa na leseni itafungiwa kushiriki Ligi.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Leseni za Klabu, Lloyd Nchunga, alisema hadi kufikia sasa klabu nyingi bado hazijafikia vigezo vya kupewa leseni.

Alisema licha ya kuhimiza suala hilo kwa miaka mitano, lakini klabu zimekuwa zikisuasua kutekeleza taratibu, huku nyingine zikiwa hazijatuma maombi kabisa.

Nchunga alisema kuna vigezo muhimu vinavyotakiwa kufuatwa ili klabu ipewe leseni, imekuwa ngumu kwa wahusika kutekeleza, hivyo wameona watoe adhabu mbalimbali.

Alivitaja baadhi ya vigezo hivyo kuwa ni klabu kuwa na uwanja wenye huduma zote muhimu, programu ya vijana, utawala bora na ofisi za kila idara, katiba na kusajiliwa.

“Hatutavumilia mtu, tumefuatilia kwa muda mrefu na klabu tulikuwa tunazisisitiza juu ya hilo, lakini imekuwa ngumu kutekeleza, sasa tunaomba muwafikishie taarifa, dirisha dogo tunazifungia,” alisema.

Alifafanua kuwa, kutokana na ukaguzi wa viwanja walivyofanya, viwanja vingi vitafungiwa na tayari wamebaini Uwanja wa Majimaji na Jamhuri Morogoro havifai.

Katika hatua nyingine, Nchunga alisema katika kikao cha kamati hiyo, kilichokaa Septemba 4, mwaka huu, kimezipiga faini ya Sh 500,000 kila mmoja klabu za  JKT Tanzania, Lipuli FC, Mbao FC, Stand United na KMC, kwa kushindwa kurudisha mrejesho baada ya kupewa utaratibu.

Pia Klabu ya African Lyon, Kagera Sugar, Mbeya City, zimepigwa faini ya Sh 1,000,000 kwa sababu hazijatuma hata maombi ya leseni.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*