googleAds

MO AWATIA KIWEWE YANGA

NA ZAITUNI KIBWANA

SIKU moja baada ya bilionea Mohammed Dewji ‘Mo’ kuanza hatua za awali za ujenzi wa Uwanja wa Simba uliopo Bunju, Dar es Salaam, Yanga wamepatwa na kiwewe wakiamini hilo ni pigo kubwa na fedheha ya aina yake kwao.

Kwa muda mrefu, Simba na Yanga zimekuwa zikiteseka kusaka viwanja vya kufanyia mazoezi na matokeo yake kujikuta zikigombania viwanja vya Chuo cha Polisi Kurasini, Boko Veterans, Chuo cha Bandari na Shule ya Sekondari Loyola.

Japo Yanga wana uwanja wao wa Kaunda uliopo klabuni kwao, katika makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, lakini umekuwa si wa kutegemea kwani wakati mwingine umekuwa ukijaa maji.

Kwa nyakati tofauti, viongozi wa klabu hizo mbili wamekuwa wakiahidi kujenga uwanja wa mazoezi kwa timu zao, lakini mara zote ahadi hizo zimekuwa zikiishia hewani.

Hatimaye, Mo ambaye ameshinda zabuni ya uwekezaji ndani ya Simba, ameamua kufanya kweli kwa kuanza kuujenga uwanja wa timu hiyo uliopo Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Juzi Mo aliposti ujumbe katika mtandao wake wa instagram akifurahia kuanza ukarabati wa uwanja huo wenye ukubwa wa ekari 20 akitamba kukamilika Februari mwakani.

Baada ya tambo hizo za Mo, wanachama wa Yanga walionekana kuguswa mno, wakitaka uchaguzi mkuu wa klabu hiyo ufanyike haraka ili viongozi watakaopatikana waweze kushughulikia suala la uwanja wao ili kuwaepusha na kebehi kutoka kwa wenzao wa Simba.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mwanachama wa Yanga, tawi la Makao Makuu Jangwani, Abdul Samadu, alisema maendeleo ya soka kwa sasa yanafanywa na watu wenye fedha, hivyo Yanga wanapaswa kufanya maamuzi magumu.

“Tunaona wenzetu Simba wanafanya mambo makubwa toka wameingia kwenye mabadiliko, Mo amekuwa anawapa kila kitu wakati sisi tunaendelea kutembeza bakuli, viongozi wanapaswa kutuambia ukweli na si kukaa kimya,” alisema.

Naye meneja wa zamani wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Boniface Clement, alisema anachokifanya Mo kinapaswa pia kufanywa na Yanga ili klabu hiyo iweze kujiendesha yenyewe.

“Klabu zinapaswa kujiendesha zenyewe ili ziweze kujitegemea na kunufaika, si kutembeza bakuli. Kuna faida kubwa ya timu kuwa na tajiri na kubadilisha mfumo wa uendeshaji,” alisema.

BINGWA lilimtafuta Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Yanga, Tobias Lingarangala, ili kuzungumzia kilio hicho cha wanachama wao, hasa kuhusu uchaguzi ambapo alisema suala hilo kwa sasa lipo chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, George Mkuchika.

“Ni kweli tunahitaji kufanya uchaguzi ili kuendana na kasi ya mabadiliko kama waliyokuwa nayo wenzetu ila masuala yote tumemwachia Mkuchika, yeye atakuwa anajua kila kitu,” alisema.

Gazeti hili lilipomtafuta Mkucha kuzungumzia hilo, muda wote simu yake iliita bila kupokewa.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*