googleAds

YONDANI ATOA SIMULIZI NZITO

NA HUSSEIN OMAR

Wakati mashabiki wa Simba wakiendelea kujiuliza ilikuwaje hadi wakashindwa kufunga bao hata moja pamoja na kuutawala mchezo dhidi ya Yanga mwishoni mwa wiki iliyopita, beki wa watani hao wa jadi, Kelvin Yondani, ametoa simulizi nzito juu ya kilichotokea katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Pambano hilo la kukata na shoka liliishia kwa wakongwe hao wa soka nchini kutoka suluhu, huku Simba wakimiliki mchezo kwa asilimia 62, lakini pia wakikosa mabao ya wazi saba, wakipata kona kumi na moja dhidi ya moja ya watani wao hao.

Lakini kwa kiasi kikubwa, kipa wa Yanga, Benno Kakolanya ndiye aliyeibuka shujaa wa mchezo huo baada ya kuokoa mikwaju hiyo saba ya Simba, tena kutoka kwa wachezaji mahiri kabisa wa Wekundu wa Msimbazi hao, Emmanuel Okwi, Meddie Kagere, Cletus Chama na Shiza Kichuya.

Wakati wapenzi wengi wa soka wakimmwagia sifa Kakolanya kwa kuwabania akina Okwi, wapo waliohusisha matokeo yale na imani za kishirikina (japo BINGWA hatuamini mambo hayo), wakidai kuwa Kagere, Okwi na Kichuya si wa kukosa mabao kama yale yaliyookolewa na kipa huyo.

Na kitendo cha Ibrahim Ajib wa Yanga kuanzisha mpira kwa kuutoa nje, waliamini yalikuwa ni maelekezo maalumu kutoka kwa ‘babu’ na ndio maana mikwaju ya washambuliaji wao ama ilitoka nje au kuishia mikononi mwa Kakolanya.

Lakini wakati mashabiki wa soka wa Simba na hata wa Yanga wakiendelea kuumiza vichwa vyao kutokana na kile kilichotokea Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yondani amekiri kuwa ni Mungu pekee aliyewanusuru na kuepuka mvua ya mabao kutoka kwa akina Kagere.

Akizungumza na BINGWA jana, Yondani alisema walipambana kufa au kupona huku wakijua wapinzani wao walikuwa wamekamilika kila idara, hivyo wangekuwa na kazi ya ziada kuwadhibiti.

“Mechi ilikuwa ngumu sana kuliko zote nilizowahi kucheza, lakini mwisho wa siku, Mungu alikuwa upande wetu, tukapata sare na kuambulia pointi moja,” alisema Yondani.

Alisema katika maisha yake yote aliyocheza soka, hajawahi kukaba kama alivyokaba katika mchezo huo uliowakutanisha vigogo hao wa soka hapa nchini, kwani alicheza kwa uwezo wake wote kuhakikisha akina Okwi na Kagere hawapati bao.

“Nashangaa watu wanasema eti tulifanya mambo ya kishirikina kisa wenzetu wamekosa mabao mengi, hapana, wao walikuwa hawana bahati, sisi tulikuwa na bahati kwa sababu tulikoswa kufungwa mabao mengi.

“Nilikaba mpaka ilifika sehemu nikasema, hapana, lakini wenzetu walipokosa yale mabao manne ya wazi, nikasema, hapa ndio imekula kwao, kazi imebaki kwetu kuhakikisha hakuna goli litakoloingia na mwisho wa siku tukafanikiwa katika hilo,” alisema Yondani.

Alisema kitendo cha Ajib kuanza mpira kwa kuupiga nje, alisema ilikuwa ni sehemu ya staili ya kuanzisha mpira ili kucheza na akili za wachezaji wa Simba kuwaondoa mchezoni na kwamba hakukuwa na kitu chochote nyuma ya pazia kama mashabiki wa wapinzani wao wanavyodhani.

Yondani ambaye uwezo wake wa kucheza umemfanya kuogopewa na washambuliaji wa timu pinzani, alisema kazi iliyopo mbele yao kwa sasa ni kuhakikisha wanashinda kila mchezo.

“Unajua tulikosa pesa (fedha) nyingi sana baada ya kukosa kuifunga Simba na kuambulia sare, si unajua ile ndio ilikuwa mechi ya hela (fedha), sasa kazi ni moja, kushinda kila mchezo ili kuwavuta matajiri,” alisisitiza.

Yanga inatarajia kushuka dimbani Jumapili kuwavaa Mbao FC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hadi sasa, Yanga wameshacheza mechi tano na kujikusanyia pointi 13 baada ya kushinda nne na kupata suluhu moja.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*