googleAds

KISA YANGA… Mbelgiji acharuka Simba

 

NA SAADA SALIM


 

KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, ameonekana kukerwa na                                                                                   kitendo cha kikosi chake kushindwa kupata ushindi dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi na hivyo kugoma kuwapumzisha wachezaji wake na badala yake kuamua kuwahenyesha vilivyo jana.

Licha ya Simba kucheza kandanda la kuvutia na kumiliki sehemu kubwa ya mchezo huo, walijikuta wakikosa nafasi zaidi ya saba za kufunga mabao, huku kikwazo chao kikubwa akitajwa kipa wa Yanga, Benno Kakolanya.

Akiamini kuwa na kikosi kilicho sheheni wachezaji wa kiwango cha juu tofauti na kilivyo cha wapinzani wao, Mbelgiji huyo anadhani wachezaji wake walizembea ndio maana walishindwa kufunga hata bao moja.

Hivyo, kocha huyo aliamua kuwapigisha kwata la maana wachezaji wake wote, wakiwamo nyota wa kigeni kwenye mazoezi yaliyofanyika Uwanja wa Boko Veterani, Dar es Salaam.

Katika mazoezi hayo ya saa moja, Aussems alionekana kuwa makini zaidi na washambuliaji wake kuhakikisha wanatumia vyema nafasi zinazotengenezwa na viungo wao, tofauti na ilivyokuwa juzi walipokosa mabao ya wazi saba.

Akizungumza na BINGWA baada ya mazoezi hayo ya jana, kocha huyo alisema ameona makosa katika mchezo huo na kuyafanyia kazi kuhakikisha washambuliaji wake wanakuwa makini kutumia nafasi wanazopata.

Alisema katika mchezo wao dhidi ya Yanga, walipata nafasi nyingi lakini washambuliaji wao hawakuwa makini kuzitumia ipasavyo nafasi hizo.

“Vijana wamecheza vizuri, lakini tumeangushwa na washambuliaji, nina imani wangekuwa watulivu na makini, tungepata ushindi kwa nafasi tulizotengeneza,” alisema.

Aussems alisema ameamua kuendelea na programu yake ya mazoezi kuhakikisha katika michezo iliyopo mbele yao, wanafanya vizuri.

Alisema kulingana na ratiba kutokuwa rafiki, anahitaji kuendelea na programu zake kwani ana muda mfupi wa kujiandaa kwani pia wanakabiliwa na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwezi ujao.

“Kikosi kina wachezaji wazuri na vijana, tunaendelea na mazoezi yetu kwani tunahitaji kufanya vizuri huko mbele, bado mechi nyingi na nina imani tutatetea ubingwa wetu,” alisema kocha huyo.

Simba imecheza mechi sita, ikishinda tatu, sare mbili na kufungwa mchezo mmoja dhidi ya Mbao FC, hivyo kujikusanyia pointi 11, wakati Yanga walioshuka dimbani mara tano, wakishinda nne na sare moja na kujikusanyia pointi 13.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*