googleAds

ALLEGRI ACHOCHEA KASI YA DYBALA, RONALDO

TURIN, Italia


 

KOCHA wa timu ya Juventus, Max Allegri, amesema anaamini washambuliaji wake, Paulo Dybala na Cristiano Ronaldo, watatengeneza ‘kombinesheni’ kali zaidi, baada ya nyota hao kuisaidia timu yao hiyo kuinyuka Bologna mabao 2-0.

Juve iliibuka na ushindi huo muhimu katika mchezo wa Ligi Kuu Italia, uliochezwa usiku wa kuamkia jana kwenye dimba la Turin.

Dybala ndiye aliyepachika bao la kwanza kabla ya Ronaldo kutoa pasi ya mwisho iliyomfikia kiungo, Blaise Matuidi, ambaye alipachika bao la pili kwa upande wa Bianconeri hao.

Kiwango hicho cha hali ya juu cha mashambulizi kilimkuna Allegri, kwani kiliisaidia Juve kunyakua ushindi wao wa sita mfululizo wa Ligi hiyo, baada ya wikiendi iliyopita kuinyuka Frosinone mabao 2-0.

Katika mchezo huo, Allegri alimwanzisha benchi straika wake mwingine, Mario Mandzukic na kuamua kuwaanzisha Ronaldo kama namba tisa, huku Dybala akitokea nyuma yake.

Kocha huyo alisema kwa kiwango walichoonesha dhidi ya Bologna, anaamini wawili hao wana nafasi ya kuwa bora zaidi, hata akiwapanga sambamba na Mandzukic.

“Nimeridhishwa na kiwango cha Dybala. Alicheza vizuri sana leo (juzi), alikuwa ni yule yule wa wikiendi iliyopita dhidi ya Frosinone. Anahitaji kuimarika zaidi na zaidi.

“Kiujumla, wote wawili (Ronaldo na Dybala) walicheza soka safi. Wakiendelea kucheza pamoja naamini wataunda safu kali ya mashambulizi kwa sababu watakuwa wameshazoeana, bado wana nafasi hiyo,” alisema Allegri.

“Nadhani pia wakianza watatu, Ronaldo, Dybala na Mandzukic, akisimama katikati, watacheza vizuri zaidi,” aliongeza kocha huyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*