MENGI APEWE SAPOTI SERENGETI BOYS


MWENYEKITI wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, ameteuliwa kuwa mlezi wa timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17, ‘Serengeti Boys’, inayotarajiwa kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika hapa nchini.

Mfanyabiashara huyo maarufu hapa nchini na Afrika, alitangazwa juzi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kupewa nafasi hiyo, huku jukumu lake la kwanza likiwa ni kufanikisha ushiriki wa timu hiyo katika fainali hizo za Afrika zitakazofanyika Aprili mwakani.

Mbali ya hilo, Mengi pia atatakiwa kufanya kila linalowezekana kuhakikisha Serengeti Boys inatwaa ubingwa wa fainali hizo za vijana.

Akizungumza katika hafla ya utambulisho wake, jijini Dar es Salaam juzi, Mengi aliwaahidi Watanzania kuiwezesha timu hiyo kufanya kweli katika fainali hizo zinazofanyika hapa nchini kwa mara ya kwanza.

“Hakuna sababu ya Serengeti Boys kutokuwa washindi, tunaamini tunaweza na timu hii itailetea Tanzania heshima kubwa. Shakira (mwanamuziki wa Colombia) aliimba ‘This time is for Africa’ wakati wa Kombe la Dunia 2010, na sisi tunasema ‘This time is for Tanzania (safari hii ni zamu ya Tanzania).

“Tuna kila kitu cha kutufanya tuwe washindi, wanachotakiwa vijana kufanya ni kujiamini. Tutafanya kila tunaloweza kuhakikisha timu inapata maandalizi ya kutosha ili iweze kufanya vizuri,” alisema.

Alimtaka kila Mtanzania kujivunia timu hiyo ya Serengeti Boys huku akiahidi kutowaangusha Watanzania kutokana na nafasi hiyo.

Kwa upande wake, Rais wa TFF, Wallace Karia, alimshukuru Mengi kwa kukubali kuwa mlezi wa Serengeti Boys, akiamini kwa ushirikiano wa kila Mtanzania, timu hiyo itafanya vizuri.

Alisema mkakati wao ni kuhakikisha timu hiyo pia inafanya vema katika fainali za Kombe la Dunia nchini Peru Oktoba mwakani na hata zile za mwaka 2026 nchini Mexico na Peru.

Tukiwa kama wadau wa soka hapa nchini, tunapenda kumpongeza Mengi kwa kukubali jukumu hilo, lakini tukiwataka Watanzania kumpa sapoti mfanyabiashara huyo.

Kama kila mmoja wetu anavyofahamu, ushiriki wetu huo unahitaji nguvu ya pamoja na si Mengi pekee, hivyo kila mmoja katika nafasi yake, aone ni vipi anaweza kutoa sapoti kwa mfanyabiashara huyo, TFF na Serikali kwa ujumla ili timu yetu iweze kutwaa ubingwa na si kuwa msindikizaji.

Ikumbukwe kuwa itakuwa ni fedheha mno kuliona kombe la fainali hizo likiyeyuka kwenye ardhi ya Tanzania wakati sisi tukiwa kama waandaaji.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*