googleAds

LIGI DARAJA LA KWANZA INAKUJA BODI YA LIGI JIPANGENI


MSIMU wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara unatarajiwa kuanza Septemba 29, mwaka huu, huku kila timu ikiwa katika maandalizi ya mwisho ya kuanza kusaka tiketi ya kucheza Ligi Kuu kwa msimu wa 2019/2020.

Mara nyingi Ligi Daraja la Kwanza inakuwa na changamoto nyingi, ikiwamo viwanja, udhamini na upangaji wa matokeo hasa kwa timu mwenyeji.

Tumeshuhudia misimu ya nyuma, baadhi ya timu zikikumbwa na kashfa ya upangaji wa matokeo na baadaye kushushwa daraja.

Lakini pamoja na changamoto hiyo, lakini waamuzi walikuwa wa kwanza kubebeshwa lawama kwa madai ya kupendelea timu mwenyeji.

Kutokana na sababu hiyo, msimu uliopita  waamuzi wengi walifungiwa kutokana na kushindwa kutafsiri kwa usahihi sheria 17 za soka.

Pamoja na changamoto ya waamuzi, lakini uzalendo umekuwa ukijitokeza baadhi ya viwanja kuhakikisha timu mwenyeji inawekewa mazingira ya kushinda michezo yake ya nyumbani ili kuweza kupanda daraja kirahisi.

Mifano ipo mingi, tumeiona kwani timu ngeni inayotoka nje ya mkoa mwingine, inafanyiwa kila hila kuhakikisha haiondoki na ushindi.

BINGWA tunasema kwamba, Bodi ya Ligi ambao ni wasimamizi wakuu wa ligi hiyo, kuanza kujipanga kikamilifu ili kuepuka malalamiko kutoka kwa timu zitakazoshiriki michuano hiyo.

Tunasema hivyo tukiwa na sababu nyingi zinazofanya Ligi Daraja la Kwanza kuwa na makandokando mengi, yakiwamo ya upangaji wa matokeo, uzalendo, lakini waamuzi kuchezesha chini ya kiwango kwa lengo la kuinufaisha timu moja.

BINGWA tunaamini Ligi Daraja ya Kwanza ina ushindani mkali pengine kuliko Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa kuwa kila timu inapambana kupanda daraja.

Kwa upande wetu BINGWA tunashauri kwamba kwa muda uliobaki kabla ya kuanza kwa ligi hiyo, itakuwa ni vizuri kwa Bodi ya Ligi kuhakikisha wanakuwa makini kufuatilia michezo itayochezwa katika viwanja vyote ili kama kutakuwa na mapungufu, basi yafanyiwe kazi mapema.

Tunarudia na kusisitiza kwamba, makondokando ya Ligi Daraja la Kwanza yasiwepo msimu mpya utakapoanza wiki ijayo, ili kupata timu bora ambazo zitapanda daraja kwa msimu ujao.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*