WACHEZAJI MBAO FC WANYANG’ANYWA SIMU

NA DAMIAN MASYENENE, MWANZA


KIPIGO cha mabao 3-2 walichokipata Mbao FC dhidi ya Simba Aprili 10, mwaka jana katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kinaonekana bado kinawanyima usingizi viongozi wa klabu hiyo hasa kutokana na mchezo wao wa leo.

Katika mchezo huo, Mbao waliokuwa wenyeji walikuwa wanaongoza kwa mabao 2-0 hadi dakika ya 82 yaliyofungwa na Evarigestus Mujwahuki na George Sangija, lakini Simba walikuja juu na kusawazisha mabao hayo.

Mabao ya Simba yalifungwa na Fredrick Blagnon na Mzamiru Yassin aliyefunga bao la ushindi dakika za lala salama, hivyo mchezo kumalizika kwa Wekundu hao wa Msimbazi kushinda mabao 3-2.

Mchezo huo ulileta simanzi katika mitaa ya Sabasaba na kupelekea mlinda mlango namba moja wa Mbao FC, Erick Ngwengwe, kusimamishwa kwa tuhuma za kuihujumu timu hiyo.

Katika kuelekea mchezo wao wa leo wa Ligi Kuu dhidi ya Simba, uongozi wa Mbao tayari umechukua tahadhari ili kuepusha hujuma kwa kuwanyang’anya simu wachezaji wake tangu Jumanne.

Wakizungumza na BINGWA baadhi ya wachezaji wa Mbao kwa masharti ya kutotajwa majina yao, walidai wamenyang’anywa simu ili kuepuka hujuma za namna yoyote pamoja na hofu ya wachezaji kurubuniwa.

Hata hivyo, Kocha Mkuu wa Mbao FC, Amri Said, alisema kikosi chake kimejiandaa vya kutosha na kipo tayari kumkabili mnyama Simba leo, huku akielezea kufurahia kurejea kwa baadhi ya wachezaji waliokosekana katika mchezo uliopita dhidi ya JKT Tanzania.

Amri ambaye pia amewahi kuichezea Simba, alisema wamekaa na wachezaji na kuzungumza nao kuhusiana na mchezo huo na pia anashukuru wameonyesha umakini katika mazoezi yao juzi katika Uwanja wa CCM Kirumba.

“Tumefanya mazoezi leo (jana), lakini tumepumzika mazoezi magumu na tumefanya ya kawaida, tumefurahi kwa asilimia kubwa kiwango ni kizuri na pia kisaikolojia tumejiandaa vyema, kikubwa ni kupata matokeo.

“Wachezaji tumekaa nao vizuri ili kurudisha akili yao sawa na hata waliokuwa majeruhi wanaendelea vizuri na hakuna atakayekosekana,” alisema Amri.

 Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza leo saa 10 jioni Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), kimetangaza viingilio vya mchezo huo ambayo katika jukwaa kuu (VVIP) ni Sh 30,000, VIP Sh 20,000, mzunguko Sh 5,000 na vijana (yosso) Sh 2,500.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*