TENGENEZA MAZINGIRA HAYA YA KUAMINIKA UPATE AMANI

Na RAMADHANI MASENGA


ILI uhusiano wenu ulete maana, inabidi kuwe na furaha na amani, bila kuaminiana baina ya wahusika mapenzi hakuna amani inayopatikana.

Kila mmoja ana dhima ya kufanya ili aaminike kwa mwenzake. Kuaminika si suala la kuonekana mtakatifu tu, ila pia limebeba maana kamili ya uhusiano wa mapenzi.

Hata siku moja haiwezi kuonekana kama mnapendana kwa dhati ikiwa kila mmoja hana imani na mwenzake. Bila imani kamili kwa mwingine hakuna mapenzi kamili zaidi ya ahadi za mdomoni zisizo na mashiko.

Jiulize, kwanini mpenzi wako anapungukiwa na imani juu yako? Angalia matendo na kauli zako. Angalia ahadi na aina ya watu unaopenda kuwa nao karibu.

Ni aghalabu sana kumfanya mwenzako kuwa na amani ikiwa aina ya watu unaokaa nao wana sifa mbaya au wanaonekana wanamazoea ya ajabu na wewe.

Kwa kuwa umeamua kuwa na huyo uliyenaye. Kuna baadhi ya mambo ni lazima ufanye. Uhakikishe awe na amani na furaha. Kama kuna mahali unahisi unasababisha imani yake juu yako iyumbe ifanyie kazi. Kama ni mazoea yaliyochupa mipaka achana nayo. Kama ni safari zisizo na maelezo ya kina pia achana nazo.

Hata siku moja safari za maana haziwezi kukosa maelezo ya kutosha. Kama zingekuwa ni safari za kazi au za maana kwako, kungekuwa na maelezo yake ya kujitosheleza. Acha kuiweka nafsi ya mwenzako katika hali ya wasiwasi. Kadri unavyoiweka nafsi yake katika hali hiyo ndivyo mwenzako anavyoteseka na wakati mwingine kujuta kwanini yupo katika uhusiano na wewe.

Hakikisha amani na utulivu vinakuwa karibu sana na mwenzako. Kauli na matendo yako vinatakiwa kubeba ujumbe mwafaka sana kwake.  Katika hali ya kujenga na kuimarisha uhusiano wako, maneno, kauli na hata marafiki zako havipaswi kuwa moja ya sababu ya kulegea uhusiano wako. Pigania uoneshe thamani yake katika misha yako. Mjali na msikilize kwa kina.

Wengi wakati mwingine wanajihisi wakiwa na hali ya kutoamini wenzao kwa sababu ya kutowajali na kuwasikiliza. Kila anachosema kama hakijapingwa kijinga kijinga, basi kitakubaliwa kinafiki. Hali kama hii unadhani inajenga picha gani kwa mwenzako?

Kweli si vyema kukubali kila kitu kutoka kwa mwenzako, ila pia si vyema kupinga jambo, hasa la kimapenzi lenye tija bora kwenu, bila maelezo ya kumtosheleza.

Kwa mfano; mwenzako kakwambia ana hamu ya kwenda na wewe mahali, badala  ya kumkubalia au kumkatalia kwa sababu za maana, unasema hujisikii kutoka, ila siku nyingine tena unatoka ila hutoki naye bali unakwenda na marafiki zako. Mwenzako akufikirie nini? Sio kama unamkwepa? Na kama unamkwepa utamzuia vipi kuamini kuwa kuna mtu mwingine anayekufanya usimuone mali kitu?

Kama ukiaminika na mpenzi wako mbali na mambo mengine ila pia utafanya nyumba yako kuwa na amani na utulivu. Kila siku kwenu vicheko, kwa sababu kama ukimwambia unampenda anajua kweli na kama ukimwambia fulani humpendi pia anajua kweli. Katika hali hiyo, ndani ya nafsi yake anajihisi na thamani na anatakiwa. Sasa vipi kama akiacha kukuamini?

Kila siku maneno yako anayawekea mashaka. Kila unapoaga kuwa unakwenda mahali kikazi anajua unakwenda kukutana na kimada. Sasa hayo maisha? Ndiyo, anakupenda, ndiyo maana anaumia, ila unatengeneza nini katika nafsi yake zaidi ya jakamoyo ambalo baadaye litageuka kuwa barafu likakaloyeyusha mapenzi yake kwako? Jenga mazingira ya mwenzako kukuona bora na kila kitu katika maisha yake.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*