JEZI NAMBA 10 YAPIGWA ‘STOP’ ARGENTINA ILI MESSI ARUDI

BUENOS AIRES, Argentina


KATIKATI mwa 2019, timu ya taifa ya Argentina itakuwa na kibarua kizito cha kuwania taji la Copa America. Haitakuwa kazi rahisi bila uwepo wa Lionel Messi.

Kutokana na changamoto waliyoigundua ipo mbele yao, mamlaka ya soka nchini humo pamoja na benchi la ufundi la Argentina, wameamua kuipumzisha jezi namba 10 lengo ni nini? Twende taratibu.

Kwa mujibu wa ripoti, timu hiyo ya taifa ya Argentina imeamua kutompa mchezaji yeyote jezi namba 10 wakiamini Messi atarudi tena katika soka la kimataifa.

Ikumbukwe kuwa Messi aliamua kustaafu soka la kimataifa baada ya timu yake hiyo ya taifa kutofanya vyema katika fainali za Kombe la Dunia mwaka huu.

Lakini, Chama cha Soka Argentina (AFA) pamoja na kocha wa muda wa timu hiyo ya taifa, Lionel Scaloni, wanahitaji mno kuona Messi akibadili uamuzi wake huo na kutinga tena jezi yake hiyo.

Mtandao wa Mundo Deportivo uliandika kwamba jaribio la Scaloni na rais wa AFA, Claudio Tapia, kumpa nafasi ya kutosha Messi, kutompa presha ya kubadili uamuzi wake na kuipumzisha jezi namba 10, lilikuwa ni la akili sana.

Iwapo Messi atashawishika, Argentina wataingia katika michuano ya Copa America mwakani na silaha za kutosha za kusaka taji la 15 la mashindano hayo makubwa katika Bara la Amerika Kusini.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*