JANGWANI WAFAFANUA SAKATA LA BANKA

SAADA SALIM NA WINFRIDA MTOI


UONGOZI wa Yanga umekiri kuwa ulipewa tahadhari na Shirikisho la Soka nchini (TFF) usimtumie kiungo wao, Mohammed Issa `Mo Banka.

Kauli hiyo ya Yanga imekuja baada ya taarifa za mchezaji huyo kufungiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), kutokana kubainika kutumia dawa za kuongeza nguvu.

Mo Banka alichukuliwa vipimo hivyo wakati wa michuano ya Kombe la Chalenji mwaka jana nchini Kenya, akiwa na kikosi cha Zanzibar Heroes.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omar Kaaya, alisema TFF walikuwa wamewaambia wasimtumie mchezaji huyo,  lakini hawakuwapa  sababu  hadi sasa wanapokuja kuzisikia.

“Nimekuwa nikiulizwa maswali mengi kuhusu mchezaji wetu Mo Banka, ukweli ni kwamba amekuwa hayupo kwenye kikosi kutokana na TFF kutuambia tusimtumie na taarifa hizo walitupa muda mrefu, lakini hawakutuambia sababu ya kutuzuia kumtumia,” alisema Kaaya.

Katika hatua nyingine, Kaaya alisema hakuna fedha yoyote waliyoipata kutoka kwa aliyekuwa mwenyekiti wao, bali wanaendelea kujiendesha kutokana na michango ya wanachama wa klabu hiyo.

Alisema tangu wameanza kuendesha zoezi hilo la uchangishaji, wamepata kiasi cha Sh milioni 29 na fedha hizo zimekuwa zikiwasaidia kuhudumia  timu.

“Fedha tunazotumia zinatokana na michango ya wanachama inayoendelea. Hao wanaosema kuna fedha tumepata kutoka kwa mwenyekiti wetu wana mpango wa kuharibu mchakato tulioanza kwa sababu wakisikia tuna hela tumepewa wataacha kuchanga,” alisema.

Kuhusu Takukuru

Kaya alifafanua kuhusu suala la klabu hiyo kuchunguzwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na kukiri kuwa watu hao walifika karibia mara tano.

“Takukuru wamefika hapa kwa ajili ya kufanya kazi yao, hatuwezi kuwazuia na sio sasa hivi tu, wamekuwa wakija mara kwa mara, inafika mara tano tukihesabu, hivyo si jambo jipya,” alisema Kaya.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*