PAMOJA ARTS GROUP KUNDI LINALOTAMANI KUENZI UTAMADUNI WA ASILI ULIOPOTEA

NA GLORY MLAY


KUNDI la sanaa la Pamoja Arts Group ni miongoni mwa makundi ya vijana wa kitanzania wenye vipaji lukuki, wakiwa ni wakali wa soka, kucheza ngoma, kuimba, maigizo pamoja na kunengua.

Kundi hilo linapatikana Kibaha Maili Moja, mkoani Pwani, likiundwa na vijana mbalimbali, baadhi yao wakiwa ni wanafunzi wa sekondari, huku wengine wakijishughulisha na kazi za nyumbani.

Pamoja Arts Group linashughulika hasa na sanaa za maonyesho ya ngoma za kitamaduni asilia katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Kundi hilo linaongozwa na Mwenyekiti wake, Abdul Muhaji, Shabi Kipande (Katibu), John Robert (Mwalimu wa ngoma), huku Hedson Rajab na Hamza Mkongo wakiwa ni wajumbe.

Wasanii wa kundi hilo ni Godwin Ferdinand, Hamza Mussa, Ram William, Naisti Emmanuel, Eliana Gaston, Theresia Sylvester, Maria Sylvester, Swaumu Rashid na Said Shaban.

Hivi karibuni, baadhi ya viongozi na wasanii wa kundi hilo walitembelea ofisi za New Habari (2006) Limited, zilizopo Sinza Kijiweni, Dar es Salaam, wazalishaji wa magazeti ya BINGWA, DIMBA, MTANZANIA, RAI na THE AFRICAN na kuzungumza mengi kuhusiana na sanaa yao na malengo yao kwa ujumla.

HISTORIA YA KUNDI

Kipande anasema kundi hilo lilianzishwa mwaka 2011 na baadhi yao kwa lengo la kurudisha heshima ya ngoma za asili hapa nchini.

Anasema baada ya kuunda kundi hilo, walilipa jina la Pamoja Arts Group, kwani waliamini kuwa, umoja ni nguvu na utengano ni dhaifu, hivyo wakiungana kwa pamoja watafanikiwa katika malengo yao.

“Pamoja Arts Group lilianza na vijana wachache, kwani wengi wao walikuwa bado hawajiamini, lakini tulijipanga kwa pamoja tukawa tunatoa matangazo mitaani na tunamshukuru Mungu wengi walijitokeza na kukafika zaidi ya 15,” anasema.

Anasema baada ya kufikia idadi hiyo, walifanikiwa kupata mwalimu wa kuwafundisha kucheza ngoma pamoja na kuimba nyimbo za kiasili za makabila mbalimbali.

“Baada ya kundi letu kuwa kubwa, tulipata mwalimu ambaye anaitwa John Robert, amekuwa msaada kwetu, amekuwa akitufundisha nyimbo za makabila ya wenzetu pamoja na uchezaji na upigaji ngoma,” anasema.

WANAANZA KAZI FASTA

Kipande anasema kundi hilo lilianza haraka sana kuandaa filamu, ambapo walifanikiwa kucheza filamu mbalimbali, ikiwamo Msitu wa Mwenda Kone na Bado Wewa, lakini hazikuweza kufika popote kutokana na kukosa fedha ya kuzisambaza.

Anasema kazi zao hizo pia hazikuwa katika ubora, kwani kamera walizotumia zilikuwa na mwanga hafifu, hivyo hazikuweza kupata soko.

“Mwanzoni tuliona kuwa filamu ndiyo kila kitu, hivyo tulianza kucheza filamu mbalimbali, lakini hazikuweza kuzaa matunda kutokana na kuwa chini ya kiwango, hivyo tuliamua kuachana na kazi hiyo ambayo tulikuwa tunatumia nguvu, lakini haikuzaa matunda.

“Ndipo tulipoamua kuingia katika kazi ya ngoma za asili, tukaona kupitia hili, tutatimiza malengo yetu na jamii pia itatukubali,” anasema.

MALENGO YAO

Kipande anasema malengo yao makubwa ni kurudisha asili ya utamaduni wa Tanzania kupitia sanaa yao, kwani umesahaulika na watu wengi wamekimbilia tamaduni za kigeni.

Anasema hakuna jipya katika sanaa za maigizo, filamu na tamthiliya, kwani wasanii wengi wamekuwa wakirudia mambo yale yale kila siku na kufanya filamu hapa nchini kurudi nyuma kila kukicha.

“Tunaamini Pamoja Arts Group litaleta maendeleo na kurejesha heshima iliyopotea ya utamaduni wetu. Tukiitumia fursa hii vyema, tutaleta mabadiliko katika utamaduni wetu wa asili na wengi watakumbuka walikotoka.

“Tunahitaji kufanya kazi kwa bidiii ili kuweza kujulikana  sehemu mbalimbali, tuna mpango wa kufanya video za kazi zetu hizi na kuanza kuzisambaza na tunaamini ndiyo njia ya kupata kipato cha kujiendesha sisi wenyewe,” anasema.

Kiongozi huyo anaomba sapoti kutoka kwa wadau, serikali na makampuni mbalimbali ili waweze kufikia malengo yao, ikiwa ni moja ya njia ya kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani pamoja na kupata ajira.

CHANGAMOTO

Kipande anasema changamoto zilizopo kwenye kikundi hicho ni ukosefu wa vitendea kazi, kama vile ngoma za kikisasa pamoja na mavazi ya asili.

Anasema wamekuwa wakitumia ngoma ambazo hazina ubora kutokana na uchanga wa kundi hilo, kwani hawana sapoti kutoka sehemu yoyote.

“Bado tunadharaulika kwakuwa kazi zetu hazijaanza kuonekana, kundi hili ni changa na linahitaji vifaa kwa ajili ya kazi yetu, tunavyotumia havina ubora na tunatumia muda mwingi sana katika hilo, tunaamini tukiwa na ngoma za kisasa, itaturahisishia kazi zaidi,” alisema.

Anasema hawana mdhamini, hivyo kusababisha kufanya kazi katika mazingira magumu, kwani wanahitaji fedha ya usafiri kwenda sehemu mbalimbali kwaajili ya kazi yao hiyo pamoja na mahitaji yao binafsi.

USHAURI WAO

Kipande amewashauri Watanzania, hasa vijana, akisema: “Ni bora kijana kujiajiri kupitia fani yake aliyonayo na kujiepusha na makundi ya mtaani, kwani siyo mazuri kwa faida ya maisha yake ya baadaye.”


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*